John 1
1 Hapo Mwanzo, Neno alikuwako; naye alikuwa na Mungu,
naye alikuwa Mungu.
2 Tangu mwanzo Neno alikuwa na Mungu.
3 Kwa njia yake vitu vyote viliumbwa; hakuna hata kiumbe kimoja kilichoumbwa
pasipo yeye.
4 Yeye alikuwa chanzo cha uhai na uhai huo ulikuwa mwanga wa watu.
5 Na mwanga huo huangaza gizani, nalo giza halikuweza kuushinda.
6 Mungu alimtuma mtu mmoja jina lake Yohane,
7 ambaye alikuja kuwaambia watu juu ya huo mwanga. Alikuja ili kwa ujumbe
wake watu wote wapate kuamini.
8 Yeye hakuwa huo mwanga, ila alikuja tu kuwaambia watu juu ya huo mwanga.
9 Huu ndio mwanga halisi, mwanga unaokuja ulimwenguni, na kuwaangazia watu
wote.
10 Basi, Neno alikuwako ulimwenguni; na kwa njia yake ulimwengu uliumbwa,
lakini ulimwengu haukumtambua.
11 Alikuja katika nchi yake mwenyewe, nao walio wake hawakumpokea.
12 Lakini wale wote waliompokea na kumwamini, hao aliwapa uwezo wa kuwa
watoto wa Mungu.
13 Hawa wamekuwa watoto wa Mungu si kwa uwezo wa kibinadamu, wala kwa nguvu
za kimwili, wala kwa mapenzi ya mtu, bali Mungu mwenyewe ndiye baba yao.
14 Naye Neno akawa mwanadamu, akakaa kwetu. Nasi tumeuona utukufu wake,
utukufu wake yeye aliye Mwana wa pekee wa Baba; amejaa neema na ukweli.
15 Yohane aliwaambia watu habari zake, akasema kwa sauti, "Huyu ndiye
niliyemtaja wakati niliposema: <Anakuja mtu mmoja baada yangu ambaye
ni mkuu kuliko mimi, maana alikuwako kabla mimi sijazaliwa.">
16 Kutokana na ukamilifu wake sisi tumepokea neema mfululizo.
17 Maana Mungu alitoa Sheria kwa njia ya Mose, lakini neema na kweli vimekuja
kwa njia ya Kristo.
18 Hakuna mtu aliyemwona Mungu wakati wowote ule. Mwana wa pekee aliye
sawa na Mungu ambaye ameungana na Baba, ndiye aliyetujulisha habari za
Mungu.
19 Huu ndio ushahidi Yohane alioutoa wakati viongozi wa Wayahudi kule Yerusalemu
walipowatuma makuhani wa Walawi kwake wamwulize: "Wewe u nani?"
20 Yohane hakukataa kujibu swali hilo, bali alisema waziwazi, "Mimi
siye Kristo."
21 Hapo wakamwuliza, "Basi, wewe ni nani? Je, wewe ni Eliya?"
Yohane akajibu, "La, mimi siye." Wakamwuliza, "Je, wewe
ni yule nabii?" Yohane akawajibu, "La!"
22 Nao wakamwuliza, "Basi, wewe ni nani? Wasema nini juu yako mwenyewe?
Tuambie, ili tuwapelekee jibu wale waliotutuma."
23 Yohane akawajibu, "Mimi ndiye yule ambaye nabii Isaya alisema habari
zake: <Sauti ya mtu imesikika jangwani: Nyoosheni njia ya Bwana.">
24 Hao watu walikuwa wametumwa na Mafarisayo.
25 Basi, wakamwuliza Yohane, "Kama wewe si Kristo, wala Eliya, wala
yule nabii, mbona wabatiza?"
26 Yohane akawajibu, "Mimi nabatiza kwa maji, lakini yuko mmoja kati
yenu, msiyemjua bado.
27 Huyo anakuja baada yangu, lakini mimi sistahili hata kumfungua kamba
za viatu vyake."
28 Mambo haya yalifanyika huko Bethania, ng'ambo ya mto Yordani ambako
Yohane alikuwa anabatiza.
29 Kesho yake, Yohane alimwona Yesu akimjia, akasema, "Huyu
ndiye Mwana-kondoo wa Mungu aondoaye dhambi ya ulimwengu!
30 Huyu ndiye niliyesema juu yake: <Baada yangu anakuja mtu mmoja aliye
mkuu zaidi kuliko mimi, maana alikuwako kabla mimi sijazaliwa!>
31 Mimi mwenyewe sikumfahamu, lakini nimekuja kubatiza kwa maji ili watu
wa Israeli wapate kumjua."
32 Huu ndio ushahidi Yohane alioutoa: "Nilimwona Roho akishuka kama
njiwa kutoka mbinguni na kutua juu yake.
33 Mimi sikumjua, lakini yule aliyenituma nikabatize watu
kwa maji alikuwa ameniambia: <Mtu yule utakayemwona Roho akimshukia
kutoka mbinguni na kukaa juu yake, huyo ndiye anayebatiza kwa Roho Mtakatifu.>
34 Mimi nimeona na ninawaambieni kwamba huyu ndiye Mwana wa Mungu."
35 Kesho yake, Yohane alikuwa tena mahali hapo pamoja na wanafunzi wake
wawili.
36 Alipomwona Yesu akipita akasema, "Tazameni! Huyu ndiye Mwana-kondoo
wa Mungu."
37 Hao wanafunzi walimsikia Yohane akisema maneno hayo, wakamfuata Yesu.
38 Basi, Yesu aligeuka, na alipowaona hao wanafunzi wanamfuata, akawauliza,
"Mnatafuta nini?" Nao wakamjibu, "Rabi (yaani Mwalimu),
unakaa wapi?"
39 Yesu akawaambia, "Njoni, nanyi mtaona." Hao wanafunzi wakamfuata,
wakaona mahali alipokuwa anakaa, wakashinda naye siku hiyo. Ilikuwa yapata
saa kumi jioni.
40 Andrea, nduguye Simoni Petro, alikuwa mmoja wa hao wawili waliokuwa
wamemsikia Yohane akisema hivyo, wakamfuata Yesu.
41 Andrea alimkuta kwanza Simoni, ndugu yake, akamwambia, "Tumemwona
Masiha" (maana yake Kristo).
42 Kisha akampeleka Simoni kwa Yesu. Naye Yesu akamtazama Simoni akasema,
"Wewe ni Simoni mwana wa Yohane. Sasa utaitwa Kefa." (maana yake
ni Petro, yaani, "Mwamba.")
43 Kesho yake Yesu aliamua kwenda Galilaya. Basi, akamkuta
Filipo, akamwambia, "Nifuate."
44 Filipo alikuwa mwenyeji wa Bethsaida, mji wa akina Andrea na Petro.
45 Naye Filipo akamkuta Nathanieli, akamwambia, "Tumemwona yule ambaye
Mose aliandika juu yake katika kitabu cha Sheria, na ambaye manabii waliandika
habari zake, yaani Yesu Mwana wa Yosefu, kutoka Nazareti."
46 Naye Nathanieli akamwuliza Filipo, "Je, kitu chema chaweza kutoka
Nazareti?" Filipo akamwambia, "Njoo uone."
47 Yesu alipomwona Nathanieli akimjia alisema juu yake, "Tazameni!
Huyo ni Mwisraeli halisi: hamna hila ndani yake."
48 Naye Nathanieli akamwuliza, "Umepataje kunijua?" Yesu akamwambia,
"Ulipokuwa chini ya mtini hata kabla Filipo hajakuita, nilikuona."
49 Hapo Nathanieli akamwambia, "Mwalimu, wewe ni Mwana wa Mungu. Wewe
ni Mfalme wa Israeli!"
50 Yesu akamwambia, "Je, umeamini kwa kuwa nimekwambia kwamba nilikuona
chini ya mtini? Utaona makubwa zaidi kuliko haya."
51 Yesu akaendelea kusema, "Nawaambieni kweli, mtaona mbingu zinafunguka
na malaika wa Mungu wakipanda na kushuka juu ya Mwana wa Mtu."
John 2
1 Siku ya tatu kulikuwa na arusi mjini Kana, mkoani Galilaya.
Mama yake Yesu alikuwapo,
2 naye Yesu alikuwa amealikwa arusini pamoja na wanafunzi wake.
3 Divai ilipokwisha, mama yake akamwambia, "Hawana divai!"
4 Yesu akamjibu, "Mama, usiniambie la kufanya. Saa yangu bado."
5 Hapo mama yake akawaambia watumishi, "Lolote atakalowaambieni, fanyeni."
6 Hapo palikuwa na mitungi sita ya mawe, ambayo kila mmoja uliweza kuchukua
kiasi cha madebe mawili au matatu. Ilikuwa imewekwa hapo kufuatana na desturi
ya Kiyahudi ya kutawadha.
7 Yesu akawaambia, "Ijazeni mitungi hiyo maji."
Nao wakaijaza mpaka juu.
8 Kisha akawaambia, "Sasa choteni mkampelekee mkuu wa karamu."
9 Mkuu wa karamu alipoonja hayo maji, kumbe yalikuwa yamegeuka kuwa divai.
Yeye hakujua ilikotoka, (lakini wale watumishi waliochota maji walijua).
Mkuu wa karamu akamwita bwana arusi,
10 akamwambia, "Kila mtu huandaa divai nzuri kwanza hata wakisha tosheka
huandaa ile hafifu. Lakini wewe umeiweka divai nzuri mpaka sasa!"
11 Yesu alifanya ishara hii ya kwanza huko Kana, Galilaya, akaonyesha utukufu
wake; nao wanafunzi wake wakamwamini.
12 Baada ya hayo, Yesu alishuka pamoja na mama yake, ndugu zake na wanafunzi
wake, wakaenda Kafarnaumu ambako walikaa kwa siku chache.
13 Sikukuu ya Wayahudi ya Pasaka ilikuwa imekaribia; hivyo
Yesu akaenda Yerusalemu.
14 Hekaluni aliwakuta watu wakiuza ng'ombe, kondoo na njiwa, na wavunja
fedha walikuwa wamekaa kwenye meza zao.
15 Akatengeneza mjeledi wa kamba, akawafukuza wote nje ya
Hekalu pamoja na kondoo na ng'ombe wao, akazimwaga sarafu za wenye kuvunja
fedha na kupindua meza zao.
16 Akawaambia wale waliokuwa wanauza njiwa, "Ondoeni vitu hivi hapa.
Msiifanye nyumba ya Baba yangu kuwa soko!"
17 Wanafunzi wake wakakumbuka kwamba Maandiko yasema: "Upendo wangu
kwa nyumba yako waniua."
18 Baadhi ya Wayahudi wakamwuliza Yesu, "Utafanya muujiza gani kuonyesha
kwamba unayo haki kufanya mambo haya?"
19 Yesu akawaambia, "Vunjeni Hekalu hili, nami nitalijenga kwa siku
tatu."
20 Hapo Wayahudi wakasema, "Hekalu hili lilijengwa kwa muda wa miaka
arobaini na sita. Je, wewe utalijenga kwa siku tatu?"
21 Lakini Yesu alikuwa anaongea juu ya Hekalu ambalo ni mwili wake.
22 Basi, alipofufuliwa kutoka wafu, wanafunzi wake walikumbuka kwamba alikuwa
amesema hayo, wakaamini Maandiko Matakatifu na yale maneno aliyokuwa akisema
Yesu.
23 Yesu alipokuwa Yerusalemu kwa sikukuu ya Pasaka, watu wengi walimwamini
walipoona ishara alizozifanya.
24 Lakini Yesu hakuwa na imani nao kwa sababu aliwajua wote.
25 Hakuhitaji kuambiwa chochote juu ya watu, maana aliyajua barabara mambo
yote yaliyomo mioyoni mwao.
John 3
1 Kulikuwa na kiongozi mmoja Myahudi, wa kikundi cha Mafarisayo,
jina lake Nikodemo.
2 Siku moja alimwendea Yesu usiku, akamwambia, "Rabi, tunajua kwamba
wewe ni mwalimu uliyetumwa na Mungu, maana hakuna mtu awezaye kufanya ishara
unazozifanya Mungu asipokuwa pamoja naye."
3 Yesu akamwambia, "Kweli nakwambia, mtu asipozaliwa upya hataweza
kuuona ufalme wa Mungu."
4 Nikodemo akamwuliza, "Mtu mzima awezaje kuzaliwa tena? Hawezi kuingia
tumboni mwa mama yake na kuzaliwa mara ya pili!"
5 Yesu akamjibu, "Kweli nakwambia, mtu asipozaliwa kwa maji na Roho,
hawezi kamwe kuingia katika ufalme wa Mungu.
6 Mtu huzaliwa kimwili kwa baba na mama, lakini huzaliwa kiroho kwa Roho.
7 Usistaajabu kwamba nimekwambia kuwa ni lazima kuzaliwa upya.
8 Upepo huvuma kuelekea upendako; waisikia sauti yake, lakini hujui unakotoka
wala unakokwenda. Ndivyo ilivyo kwa mtu aliyezaliwa kwa Roho."
9 Nikodemo akamwuliza, "Mambo haya yanawezekanaje?"
10 Yesu akamjibu, "Je, wewe ni mwalimu katika Israel na huyajui mambo
haya?
11 Kweli nakwambia, sisi twasema tunayoyajua na kushuhudia tuliyoyaona,
lakini ninyi hamkubali ujumbe wetu.
12 Ikiwa nimewaambieni mambo ya kidunia nanyi hamniamini, mtawezaje kuamini
nikiwaambieni mambo ya mbinguni?
13 Hakuna mtu aliyepata kwenda juu mbinguni isipokuwa Mwana wa Mtu ambaye
ameshuka kutoka mbinguni.
14 "Kama vile Mose alivyomwinua juu nyoka wa shaba kule jangwani,
naye Mwana wa Mtu atainuliwa juu vivyo hivyo,
15 ili kila anayemwamini awe na uzima wa milele.
16 Maana Mungu aliupenda ulimwengu hivi hata akamtoa Mwana wake wa pekee,
ili kila amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele.
17 Maana Mungu hakumtuma Mwanae ulimwenguni ili auhukumu ulimwengu, bali
aukomboe ulimwengu.
18 "Anayemwamini Mwana hahukumiwi; asiyemwamini amekwisha hukumiwa
kwa sababu hakumwamini Mwana wa pekee wa Mungu.
19 Na hukumu yenyewe ndiyo hii: Mwanga umekuja ulimwenguni lakini watu
wakapenda giza kuliko mwanga, kwani matendo yao ni maovu.
20 Kila mtu atendaye maovu anauchukia mwanga, wala haji kwenye mwanga,
maana hapendi matendo yake maovu yamulikwe.
21 Lakini mwenye kuuzingatia ukweli huja kwenye mwanga, ili matendo yake
yaonekane yametendwa kwa kumtii Mungu."
22 Baada ya hayo, Yesu alifika mkoani Yudea pamoja na wanafunzi wake. Alikaa
huko pamoja nao kwa muda, akibatiza watu.
23 Yohane pia alikuwa akibatiza watu huko Ainoni, karibu na Salemu, maana
huko kulikuwa na maji mengi. Watu walimwendea, naye akawabatiza.
24 (Wakati huo Yohane alikuwa bado hajafungwa gerezani.)
25 Ubishi ulitokea kati ya baadhi ya wanafunzi wa Yohane na Myahudi mmoja
kuhusu desturi za kutawadha.
26 Basi, wanafunzi hao wakamwendea Yohane na kumwambia, "Mwalimu,
yule mtu aliyekuwa pamoja nawe ng'ambo ya Yordani na ambaye wewe ulimshuhudia,
sasa naye anabatiza, na watu wote wanamwendea."
27 Yohane akawaambia, "Mtu hawezi kuwa na kitu asipopewa na Mungu.
28 Nanyi wenyewe mwaweza kushuhudia kuwa nilisema: <Mimi siye Kristo,
lakini nimetumwa ili nimtangulie!>
29 Bibiarusi ni wake bwanaarusi, lakini rafiki yake bwana arusi, anayesimama
na kusikiliza, hufurahi sana anapomsikia bwana arusi akisema. Ndivyo furaha
yangu ilivyokamilishwa.
30 Ni lazima yeye azidi kuwa maarufu, na mimi nipungue.
31 "Anayekuja kutoka juu ni mkuu kuliko wote; atokaye duniani ni wa
dunia, na huongea mambo ya kidunia. Lakini anayekuja kutoka mbinguni ni
mkuu kuliko wote.
32 Yeye husema yale aliyoyaona na kuyasikia, lakini hakuna mtu anayekubali
ujumbe wake.
33 Lakini mtu yeyote anayekubali ujumbe wake anathibitisha kwamba Mungu
ni kweli.
34 Yule aliyetumwa na Mungu husema maneno ya Mungu, maana Mungu humjalia
mtu huyo Roho wake bila kipimo.
35 Baba anampenda Mwana na amemkabidhi vitu vyote.
36 Anayemwamini Mwana anao uzima wa milele; asiyemtii Mwana hatakuwa na
uzima wa milele, bali ghadhabu ya Mungu hubaki juu yake."
John 4
1 Mafarisayo walisikia kwamba Yesu alikuwa anabatiza na
kuwapata wanafunzi wengi kuliko Yohane.
2 (Lakini ukweli ni kwamba Yesu hakuwa anabatiza ila wanafunzi wake.)
3 Basi, Yesu aliposikia hayo, alitoka Yudea akarudi Galilaya;
4 na katika safari hiyo ilimbidi apitie Samaria.
5 Basi, akafika Sukari, mji mmoja wa Samaria, karibu na shamba ambalo Yakobo
alikuwa amempa mwanawe, Yosefu.
6 Mahali hapo palikuwa na kisima cha Yakobo, naye Yesu, kutokana na uchovu
wa safari, akaketi kando ya kisima. Ilikuwa yapata saa sita mchana.
7 Basi, mwanamke mmoja Msamaria akafika kuteka maji. Yesu akamwambia, "Nipatie
maji ninywe."
8 (Wakati huo wanafunzi wake walikuwa wamekwenda mjini kununua chakula.)
9 Lakini huyo mwanamke akamwambia, "Wewe ni Myahudi; mimi ni mwanamke
Msamaria! Unawezaje kuniomba maji?" (Wayahudi hawakuwa na ushirikiano
na Wasamaria katika matumizi ya vitu.)
10 Yesu akamjibu, "Kama tu ungalijua zawadi ya Mungu na ni nani anayekwambia:
<Nipatie maji ninywe,> ungalikwisha mwomba, naye angekupa maji yaliyo
hai."
11 Huyo mama akasema, "Mheshimiwa, wewe huna chombo cha kutekea maji,
nacho kisima ni kirefu; utapata wapi maji yaliyo hai?
12 Au, labda wewe wajifanya mkuu kuliko babu yetu Yakobo? Yeye alitupa
sisi kisima hiki; na yeye mwenyewe, watoto wake na mifugo yake walikunywa
maji ya kisima hiki."
13 Yesu akamjibu, "Kila anayekunywa maji haya ataona kiu tena.
14 Lakini atakayekunywa maji nitakayompa mimi, hataona kiu milele. Maji
nitakayompa yatakuwa ndani yake chemchemi ya maji ya uzima na kumpatia
uzima wa milele."
15 Huyo mwanamke akamwambia, "Mheshimiwa, nipe maji hayo ili nisione
kiu tena; nisije tena mpaka hapa kuteka maji."
16 Yesu akamwambia, "Nenda ukamwite mumeo uje naye hapa."
17 Huyo mwanamke akamwambia, "Mimi sina mume." Yesu akamwambia,
"Umesema kweli, kwamba huna mume.
18 Maana umekuwa na waume watano, na huyo unayeishi naye sasa si mume wako.
Hapo umesema kweli."
19 Huyo Mwanamke akamwambia, "Mheshimiwa, naona ya kuwa wewe u nabii.
20 Babu zetu waliabudu juu ya mlima huu, lakini ninyi mwasema
kwamba mahali pa kumwabudu Mungu ni kule Yerusalemu."
21 Yesu akamwambia, "Niamini; wakati unakuja ambapo hamtamwabudu Baba
juu ya mlima huu, wala kule Yerusalemu.
22 Ninyi Wasamaria mnamwabudu yule msiyemjua, lakini sisi tunamjua huyo
tunayemwabudu, kwa maana wokovu unatoka kwa Wayahudi.
23 Lakini wakati unakuja, tena umekwisha fika, ambapo wanaoabudu kweli,
watamwabudu Baba kwa nguvu ya Roho; watu wanaomwabudu hivyo ndio Baba anaotaka.
24 Mungu ni Roho, na watu wataweza tu kumwabudu kweli kwa nguvu ya Roho
wake."
25 Huyo mama akamwambia, "Najua kwamba Masiha, aitwaye Kristo, anakuja.
Atakapokuja atatujulisha kila kitu."
26 Yesu akamwambia, "Mimi ninayesema nawe, ndiye."
27 Hapo wanafunzi wake wakarudi, wakastaajabu sana kuona anaongea na mwanamke.
Lakini hakuna mtu aliyesema: "Unataka nini?" au, "Kwa nini
unaongea na mwanamke?"
28 Huyo mama akauacha mtungi wake pale, akaenda mjini na kuwaambia watu,
29 "Njoni mkamwone mtu aliyeniambia mambo yote niliyotenda! Je, yawezekana
kuwa yeye ndiye Kristo?"
30 Watu wakatoka mjini, wakamwendea Yesu.
31 Wakati huohuo wanafunzi wake walikuwa wanamsihi Yesu: "Mwalimu,
ule chakula."
32 Lakini Yesu akawaambia, "Mimi ninacho chakula msichokijua ninyi."
33 Wanafunzi wake wakaulizana, "Je, kuna mtu aliyemletea chakula?"
34 Yesu akawaambia, "Chakula changu ni kufanya anachotaka yule aliyenituma
na kuitimiza kazi yake.
35 Ninyi mwasema: <Bado miezi minne tu, na wakati wa mavuno utafika!>
Lakini mimi nawaambieni, yatazameni mashamba; mazao yako tayari kuvunwa.
36 Mvunaji anapata mshahara wake, na anakusanya mavuno kwa ajili ya uzima
wa milele; hivyo mpandaji na mvunaji watafurahi pamoja.
37 Kwa sababu hiyo msemo huu ni kweli: <Mmoja hupanda na mwingine huvuna.>
38 Mimi nimewatuma mkavune mavuno ambayo hamkuyatolea jasho, wengine walifanya
kazi, lakini ninyi mnafaidika kutokana na jasho lao."
39 Wasamaria wengi wa kijiji kile waliamini kwa sababu ya maneno aliyosema
huyo mama: "Ameniambia mambo yote niliyofanya."
40 Wasamaria walimwendea Yesu wakamwomba akae nao; naye akakaa hapo siku
mbili.
41 Watu wengi zaidi walimwamini kwa sababu ya ujumbe wake.
42 Wakamwambia yule mama, "Sisi hatuamini tu kwa sababu ya maneno
yako; sisi wenyewe tumesikia, na tunajua kwamba huyu ndiye kweli Mwokozi
wa ulimwengu."
43 Baada ya siku mbili Yesu aliondoka hapo, akaenda Galilaya.
44 Maana Yesu mwenyewe alisema waziwazi kwamba, "Nabii hapati heshima
katika nchi yake."
45 Basi, alipofika Galilaya, Wagalilaya wengi walimkaribisha. Maana nao
pia walikuwa kwenye sikukuu ya Pasaka, wakayaona mambo yote Yesu aliyotenda
huko Yerusalemu wakati wa sikukuu hiyo.
46 Yesu alifika tena huko mjini Kana, mkoani Galilaya, mahali alipogeuza
maji kuwa divai. Kulikuwa na ofisa mmoja aliyekuwa na mtoto mgonjwa huko
Kafarnaumu.
47 Basi, huyo ofisa aliposikia kuwa Yesu alikuwa ametoka Yudea na kufika
Galilaya, alimwendea akamwomba aende kumponya mtoto wake aliyekuwa mgonjwa
mahututi.
48 Yesu akamwambia, "Msipoona ishara na maajabu hamtaamini!"
49 Huyo ofisa akamwambia, "Mheshimiwa, tafadhali twende kabla mwanangu
hajafa."
50 Yesu akamwambia, "Nenda tu, mwanao yu mzima." Huyo mtu akaamini
maneno ya Yesu, akaenda zake.
51 Alipokuwa bado njiani, watumishi wake walikutana naye, wakamwambia kwamba
mwanawe alikuwa mzima.
52 Naye akawauliza saa mtoto alipopata nafuu; nao wakamwambia, "Jana
saa saba mchana, homa ilimwacha."
53 Huyo baba akakumbuka kwamba ilikuwa ni saa ileile ambapo Yesu alimwambia:
"Mwanao yu mzima." Basi, yeye akaamini pamoja na jamaa yake yote.
54 Hii ilikuwa ishara ya pili aliyoifanya Yesu alipokuwa anatoka Yudea
kwenda Galilaya.
John 5
1 Baada ya hayo kulikuwa na sikukuu ya Wayahudi, naye
Yesu akaenda Yerusalemu.
2 Huko Yerusalemu, karibu na mlango uitwao Mlango wa Kondoo, kulikuwa na
bwawa la maji liitwalo kwa Kiebrania Bethzatha, ambalo lilikuwa na baraza
tano zenye matao.
3 Humo barazani mlikuwa na wagonjwa wengi wamekaa: vipofu, viwete na waliopooza.
Walikuwa wakingojea maji yatibuliwe,
4 maana mara kwa mara malaika alishuka majini nyakati fulani na kuyatibua.
Mtu yeyote aliyekuwa wa kwanza kuingia majini baada ya maji kutibuliwa,
alipona ugonjwa wowote aliokuwa nao.
5 Basi, hapo palikuwa na mtu mmoja aliyekuwa mgonjwa kwa muda wa miaka
thelathini na minane.
6 Naye alipomwona huyo mtu amelala hapo, akatambua kwamba alikuwa amekaa
hapo kwa muda mrefu, akamwuliza, "Je, wataka kupona?"
7 Naye akajibu, "Mheshimiwa, mimi sina mtu wa kunipeleka majini wakati
yanapotibuliwa. Kila nikijaribu kuingia, mtu mwingine hunitangulia."
8 Yesu akamwambia, "Inuka, chukua mkeka wako utembee."
9 Mara huyo mtu akapona, akachukua mkeka wake, akatembea. Jambo hili lilifanyika
siku ya Sabato.
10 Kwa hiyo baadhi ya Wayahudi wakamwambia huyo mtu aliyeponywa, "Leo
ni Sabato, si halali kubeba mkeka wako."
11 Lakini yeye akawaambia, "Yule mtu aliyeniponya ndiye aliyeniambia:
<Chukua mkeka wako, tembea.">
12 Nao wakamwuliza, "Huyo mtu aliyekwambia: <Chukua mkeka wako,
tembea,> ni nani?"
13 Lakini yeye hakumjua huyo mtu aliyemponya, maana Yesu alikuwa amekwisha
ondoka mahali hapo, kwani palikuwa na umati mkubwa wa watu.
14 Basi, baadaye Yesu alimkuta huyo aliyeponywa Hekaluni, akamwambia, "Sasa
umepona; usitende dhambi tena, usije ukapatwa na jambo baya zaidi."
15 Huyo mtu akaenda, akawaambia viongozi wa Wayahudi kwamba Yesu ndiye
aliyemponya.
16 Kwa vile Yesu alifanya jambo hilo siku ya Sabato, Wayahudi walianza
kumdhulumu.
17 Basi, Yesu akawaambia, "Baba yangu anafanya kazi daima, nami pia
nafanya kazi."
18 Kwa sababu ya maneno haya, viongozi wa Wayahudi walizidi kutafuta njia
ya kumwua Yesu: si kwa kuwa aliivunja Sheria ya Sabato tu, bali pia kwa
kuwa alisema kwamba Mungu ni Baba yake, na hivyo akajifanya sawa na Mungu.
19 Yesu akawaambia, "Kweli nawaambieni, Mwana hawezi kufanya kitu
peke yake; anaweza tu kufanya kile anachomwona Baba akikifanya. Maana kile
anachofanya Baba, Mwana hukifanya vilevile.
20 Baba ampenda Mwana, na humwonyesha kila kitu anachokifanya yeye mwenyewe,
tena atamwonyesha mambo makuu kuliko haya, nanyi mtastaajabu.
21 Kama vile Baba huwafufua wafu na kuwapa uzima, vivyo hivyo naye Mwana
huwapa uzima wale anaopenda.
22 Baba hamhukumu mtu yeyote; shughuli yote ya hukumu amemkabidhi Mwana,
23 ili watu wote wamheshimu Mwana kama vile wanavyomheshimu Baba. Asiyemheshimu
Mwana hamheshimu Baba ambaye amemtuma.
24 "Kweli nawaambieni, anayesikia neno langu, na kumwamini yule aliyenituma,
anao uzima wa milele. Hatahukumiwa kamwe, bali amekwisha pita kutoka kifo
na kuingia katika uzima.
25 Kweli nawaambieni, wakati unakuja, tena umekwisha fika, ambapo wafu
wataisikia sauti ya Mwana wa Mungu, nao watakaoisikia, wataishi.
26 Kama vile Baba alivyo asili ya uhai, ndivyo pia alivyomjalia Mwanawe
kuwa asili ya uhai.
27 Tena amempa mamlaka ya kuhukumu kwa sababu yeye ni Mwana wa Mtu.
28 Msistaajabie jambo hili; maana wakati unakuja ambapo wote waliomo makaburini
wataisikia sauti yake,
29 nao watafufuka: wale waliotenda mema watafufuka na kuishi, na wale waliotenda
maovu watafufuka na kuhukumiwa.
30 "Mimi siwezi kufanya kitu kwa uwezo wangu mwenyewe. Mimi nina hukumu
kama ninavyosikia kutoka kwa Baba, nayo hukumu yangu ni ya haki. Nia yangu
si kufanya nipendavyo mwenyewe, bali apendavyo yule aliyenituma.
31 Nikijishuhudia mimi mwenyewe, ushahidi wangu hauwezi kukubaliwa kuwa
wa kweli.
32 Lakini yuko mwingine ambaye hutoa ushahidi juu yangu, nami najua kwamba
yote anayosema juu yangu ni ya kweli.
33 Ninyi mlituma ujumbe kwa Yohane naye aliushuhudia ukweli.
34 Si kwamba mimi nautegemea ushahidi wa wanadamu, lakini nasema mambo
haya ili mpate kuokolewa.
35 Yohane alikuwa kama taa iliyokuwa ikiwaka na kuangaza, nanyi mlikuwa
tayari kufurahia mwanga huo kwa kitambo.
36 Lakini mimi nina ushahidi juu yangu ambao ni mkuu zaidi kuliko ule wa
Yohane. Kwa maana kazi ninazofanya, kazi alizonipa Baba nizifanye, ndizo
zinazonishuhudia kwamba Baba ndiye aliyenituma.
37 Naye Baba aliyenituma hunishuhudia. Ninyi hamjapata kamwe kusikia sauti
yake, wala kuuona uso wake,
38 na ujumbe wake haukai ndani yenu maana hamkumwamini yule aliyemtuma.
39 Ninyi huyachunguza Maandiko Matakatifu mkidhani kwamba
ndani yake mtapata uzima wa milele; na kumbe maandiko hayohayo yananishuhudia!
40 Hata hivyo, ninyi hamtaki kuja kwangu ili mpate uzima.
41 "Shabaha yangu si kupata sifa kutoka kwa watu.
42 Lakini nawajua ninyi, najua kwamba upendo kwa Mungu haumo mioyoni mwenu.
43 Mimi nimekuja kwa mamlaka ya Baba yangu, lakini hamnipokei; bali mtu
mwingine akija kwa mamlaka yake mwenyewe, mtampokea.
44 Mwawezaje kuamini, hali ninyi mnapenda kupokea sifa kutoka kwenu ninyi
wenyewe, wala hamtafuti sifa kutoka kwake yeye aliye peke yake Mungu?
45 Msifikiri kwamba mimi nitawashtaki kwa Baba. Mose ambaye ninyi mmemtumainia
ndiye atakayewashtaki.
46 Kama kweli mngemwamini Mose, mngeniamini na mimi pia; maana Mose aliandika
juu yangu.
47 Lakini hamuyaamini yale aliyoandika, mtawezaje basi, kuamini maneno
yangu?"
John 6
1 Baada ya hayo, Yesu alivuka ziwa Galilaya (au Ziwa Tiberia).
2 Umati mkubwa wa watu ulimfuata kwa sababu watu hao walikuwa wameona ishara
alizokuwa akifanya kwa kuwaponya wagonjwa.
3 Yesu alipanda mlimani, akaketi pamoja na wanafunzi wake.
4 Sikukuu ya Wayahudi iitwayo Pasaka ilikuwa imekaribia.
5 Basi, Yesu na alipotazama na kuona umati wa watu ukija kwake, alimwambia
Filipo, "Tununue wapi mikate ili watu hawa wapate kula?"
6 (Alisema hivyo kwa kumjaribu Filipo, kwani alijua mwenyewe atakalofanya.)
7 Filipo akamjibu, "Mikate ya denari mia mbili za fedha haiwatoshi
watu hawa hata kama ila mmoja atapata kipande kidogo tu!"
8 Mmoja wa wanafunzi wake aitwaye Andrea, nduguye Simoni
Petro, akamwambia,
9 "Yupo hapa mtoto mmoja aliye na mikate mitano ya shayiri na samaki
wawili; lakini hivi vyatosha nini kwa watu wengi kama hawa?"
10 Yesu akasema, "Waketisheni watu." Palikuwa na nyasi tele mahali
hapo. Basi, watu wakaketi, jumla yapata wanaume elfu tano.
11 Yesu akaitwaa ile mikate, akamshukuru Mungu, akawagawia watu waliokuwa
wameketi; akafanya vivyo hivyo na wale samaki, kila mtu akapata kadiri
alivyotaka.
12 Watu waliposhiba Yesu akawaambia wanafunzi wake, "Kusanyeni vipande
vilivyobaki visipotee."
13 Basi, wakakusanya vipande vya mikate ya shayiri walivyobakiza wale watu
waliokula, wakajaza vikapu kumi na viwili.
14 Watu walipoiona ishara hiyo aliyoifanya Yesu, wakasema, "Hakika
huyu ndiye nabii anayekuja ulimwenguni."
15 Yesu akajua ya kuwa watu walitaka kumchukua wamfanye mfalme, akaondoka
tena, akaenda mlimani peke yake.
16 Ilipokuwa jioni wanafunzi wake waliteremka hadi ziwani,
17 wakapanda mashua ili wavuke kwenda Kafarnaumu. Giza lilikuwa limeingia,
na Yesu alikuwa hajawafikia bado.
18 Ziwa likaanza kuchafuka kwa sababu upepo mkali ulikuwa
unavuma.
19 Wanafunzi walipokuwa wamekwenda umbali wa kilomita tano au sita, walimwona
Yesu akitembea juu ya maji, anakaribia mashua; wakaogopa sana.
20 Yesu akawaambia, "Ni mimi, msiogope!"
21 Walifurahi kumchukua Yesu katika mashua; na mara mashua ikawasili nchi
kavu walipokuwa wanakwenda.
22 Kesho yake umati wa watu wale waliobaki upande wa pili wa ziwa walitambua
kwamba kulikuwa na mashua moja tu pale, na Yesu hakuingia katika mashua
pamoja na wanafunzi wake, ila wanafunzi hao walikuwa wamekwenda zao peke
yao.
23 Mashua nyingine kutoka Tiberia zilifika mahali hapo watu walipokula
ile mikate, Bwana alipokwisha mshukuru Mungu.
24 Basi, hao watu walipogundua kwamba Yesu na wanafunzi wake hawakuwapo
mahali hapo, walipanda mashua, wakaenda Kafarnaumu wakimtafuta.
25 Wale watu walipomkuta Yesu ng'ambo ya pili wa ziwa walimwuliza, "Mwalimu,
ulifika lini hapa?"
26 Yesu akawajibu, "Kweli nawaambieni, mnanitafuta si kwa kuwa mmeona
ishara, bali kwa sababu mlikula ile mikate mkashiba.
27 Msikishughulikie chakula kiharibikacho; kishugulikieni chakula kidumucho
kwa ajili ya uzima wa milele. Mwana wa Mtu ambaye Baba amemthibitisha atawapeni
chakula hicho."
28 Wao wakamwuliza, "Tufanye nini ili tuweze kuzitenda kazi za Mungu?"
29 Yesu akawajibu, "Hii ndiyo kazi anayotaka Mungu muifanye: kumwamini
yule aliyemtuma."
30 Hapo wakamwambia, "Utafanya ishara gani ili tuione
tupate kukuamini? Utafanya kitu gani?
31 Wazee wetu walikula mana kule jangwani, kama yasemavyo Maandiko: <Aliwalisha
mkate kutoka mbinguni.">
32 Yesu akawaambia, "Kweli nawaambieni, Mose hakuwapeni mkate kutoka
mbinguni; Baba yangu ndiye awapaye ninyi mkate halisi kutoka mbinguni.
33 Maana mkate wa Mungu ni yule ashukaye kutoka mbinguni na aupaye ulimwengu
uzima."
34 Basi, wakamwambia, "Mheshimiwa, tupe daima mkate huo."
35 Yesu akawaambia, "Mimi ndimi mkate wa uzima. Anayekuja kwangu hataona
njaa; anayeniamini hataona kiu kamwe.
36 Lakini niliwaambieni kwamba ingawa mmeniona hamniamini.
37 Wote anaonipa Baba watakuja kwangu; nami sitamtupa nje yeyote anayekuja
kwangu,
38 kwani nimeshuka kutoka mbinguni si kwa ajili ya kufanya matakwa yangu,
ila kutimiza matakwa ya yule aliyenituma.
39 Na matakwa ya yule aliyenituma ndiyo haya: nisimpoteze hata mmoja kati
ya wale alionipa, ila niwafufue wote Siku ya mwisho.
40 Maana anachotaka Baba yangu ndicho hiki: kila amwonaye Mwana na kumwamini
awe na uzima wa milele; nami nitamfufua Siku ya mwisho."
41 Basi, Wayahudi wakaanza kunung'unika kwa kuwa alisema: "Mimi ni
mkate ulioshuka kutoka mbinguni."
42 Wakasema, "Je, huyu si mwana wa Yosefu? Tunawajua baba yake na
mama yake! Basi, anawezaje kusema kwamba ameshuka kutoka mbinguni?"
43 Yesu akawaambia, "Acheni kunung'unika ninyi kwa ninyi.
44 Hakuna mtu awezaye kuja kwangu, Baba aliyenituma asipomvuta kwangu;
nami nitamfufua mtu huyo Siku ya mwisho.
45 Manabii wameandika: <Watu wote watafundishwa na Mungu.> Kila mtu
anayemsikia Baba na kujifunza kutoka kwake, huja kwangu.
46 Hii haina maana kwamba yupo mtu aliyemwona Baba, isipokuwa yule aliyetoka
kwa Mungu; huyo ndiye aliyemwona Baba.
47 Kweli, nawaambieni, anayeamini anao uzima wa milele.
48 Mimi ni mkate wa uzima.
49 Wazee wenu walikula mana kule jangwani, lakini walikufa.
50 Huu ndio mkate kutoka mbinguni; mkate ambao anayekula hatakufa.
51 Mimi ni mkate hai ulioshuka kutoka mbinguni. Mtu yeyote akila mkate
huu ataishi milele. Na mkate nitakaompa ni mwili wangu ninaoutoa kwa ajili
ya uzima wa ulimwengu."
52 Ndipo Wayahudi wakaanza kubishana kati yao:
53 Yesu akawaambia, "Kweli nawaambieni, msipokula mwili wa Mwana wa
Mtu na kunywa damu yake, hamtakuwa na uzima ndani yenu.
54 Anayekula mwili wangu na kunywa damu yangu anao uzima wa milele nami
nitamfufua siku ya mwisho.
55 Maana mwili wangu ni chakula cha kweli, na damu yangu ni kinywaji cha
kweli.
56 Aulaye mwili wangu na kunywa damu yangu, akaa ndani yangu, nami nakaa
ndani yake.
57 Baba aliye hai alinituma, nami naishi kwa sababu yake; vivyo hivyo anilaye
mimi ataishi pia kwa sababu yangu.
58 Basi, huu ndio mkate ulioshuka kutoka mbinguni; si kama mana waliyokula
babu zetu, wakafa. Aulaye mkate huu ataishi milele."
59 Yesu alisema hayo alipokuwa akifundisha katika sunagogi kule Kafarnaumu.
60 Basi, wengi wa wafuasi wake waliposikia hayo, wakasema, "Haya ni
mambo magumu! Nani awezaye kuyasikiliza?"
61 Yesu alijua bila kuambiwa na mtu kwamba wanafunzi wake walikuwa wananung'unika
juu ya jambo hilo, akawauliza, "Je, jambo hili linawafanya muwe na
mashaka?
62 Itakuwaje basi, mtakapomwona Mwana wa Mtu akipanda kwenda kule alikokuwa
kwanza?
63 Roho ndiye atiaye uzima; binadamu peke yake hawezi. Maneno niliyowaambieni
ni Roho, ni uzima.
64 Hata hivyo, wako baadhi yenu wasioamini." (Yesu alisema hivyo kwani
alijua tangu mwanzo ni kina nani wasioamini, na pia ni nani atakayemsaliti.)
65 Kisha akasema, "Ndiyo maana niliwaambieni kwamba hakuna awezaye
kuja kwangu asipowezeshwa na Baba yangu."
66 Kutokana na hayo, wengi wa wafuasi wake walirudi nyuma wasiandamane
naye tena.
67 Basi, Yesu akawauliza wale kumi na wawili, "Je, nanyi pia mwataka
kwenda zenu?"
68 Simoni Petro akamjibu, "Bwana, tutakwenda kwa nani? Wewe unayo
maneno yaletayo uzima wa milele.
69 Sisi tunaamini, na tunajua kwamba wewe ndiwe yule Mtakatifu wa Mungu."
70 Yesu akawaambia, "Je, sikuwachagua ninyi kumi na wawili? Hata hivyo,
mmoja wenu ni Ibilisi!"
71 Yesu alisema hayo juu ya Yuda, mwana wa Simoni Iskarioti; maana huyu
alikuwa ndiye atakayemsaliti, ingawa alikuwa mmoja wa wale kumi na wawili.
John 7
1 Baada ya hayo, Yesu alikuwa akitembea katika Galilaya.
Hakutaka kutembea mkoani Yudea kwa sababu viongozi wa Wayahudi walikuwa
wanataka kumwua.
2 Sikukuu ya Vibanda ya Wayahudi ilikuwa imekaribia.
3 Basi ndugu zake wakamwambia, "Ondoka hapa uende Yudea ili wanafunzi
wako wazione kazi unazozifanya.
4 Mtu hafanyi mambo kwa siri kama anataka kujulikana kwa watu. Maadam unafanya
mambo haya, basi, jidhihirishe kwa ulimwengu."
5 (Hata ndugu zake hawakumwamini!)
6 Basi, Yesu akawaambia, "Wakati wangu ufaao haujafika bado. Lakini
kwenu ninyi kila wakati unafaa.
7 Ulimwengu hauwezi kuwachukia ninyi, lakini mimi wanichukia kwa sababu
mimi nauambia wazi kwamba matendo yake ni maovu.
8 Ninyi nendeni kwenye sikukuu hiyo. Mimi siendi kwenye sikukuu hiyo, maana
saa yangu ifaayo haijafika."
9 Alisema hayo kisha akabaki huko Galilaya.
10 Baada ya ndugu zake kwenda kwenye sikukuu, Yesu naye alikwenda, lakini
hakuenda kwa hadhara bali kwa siri.
11 Viongozi wa Wayahudi walikuwa wanamtafuta kwenye sikukuu hiyo; Wakauliza:
"Yuko wapi?"
12 Kulikuwa na minong'ono mingi katika umati wa watu. Baadhi yao walisema,
"Ni mtu mwema." Wengine walisema, "La! Anawapotosha watu."
13 Hata hivyo hakuna mtu aliyethubutu kusema, habari zake hadharani kwa
kuwaogopa viongozi wa Wayahudi.
14 Sikukuu hiyo ilipofikia katikati, Yesu naye alikwenda Hekaluni, akaanza
kufundisha.
15 Basi, Wayahudi wakashangaa na kusema "Mtu huyu amepataje elimu
naye hakusoma shuleni?"
16 Hapo Yesu akawajibu, "Mafundisho ninayofundisha si yangu, bali
ni yake yeye aliyenituma.
17 Mtu anayependa kufanya yale anayotaka Mungu, atajua kama mafundisho
yangu yametoka kwa Mungu, au mimi najisemea tu mwenyewe.
18 Yeye anayejisemea tu mwenyewe anatafuta sifa yake mwenyewe; lakini anayetafuta
sifa ya yule aliyemtuma, huyo ni mwaminifu, na ndani yake hamna uovu wowote.
19 Je, Mose hakuwapeni Sheria? Hata hivyo, hakuna hata mmoja wenu anayeishika
Sheria. Kwa nini mnataka kuniua?"
20 Hapo watu wakamjibu, "Una wazimu wewe! Nani anataka kukuua?"
21 Yesu akawajibu, "Kuna jambo moja nililofanya, nanyi mnalistaajabia.
22 Mose aliwapeni ile desturi ya kutahiri. (Si kwamba desturi hiyo ilitoka
kwa Mose, bali ilitoka kwa mababu). Sasa ninyi humtahiri mtu hata siku
ya Sabato.
23 Ikiwa basi, mtu hutahiriwa hata siku ya Sabato kusudi Sheria ya Mose
isivunjwe, mbona mnanikasirikia kwa sababu nimemfanya mtu kuwa mzima kabisa
siku ya Sabato?
24 Msihukumu mambo kwa nje tu; toeni hukumu ya haki."
25 Baadhi ya watu wa Yerusalemu walisema, "Je, yule mtu wanayemtafuta
wamuue si huyu?
26 Tazameni sasa! Anawaonya hadharani, wala hakuna mtu anayemwambia hata
neno. Je, yawezekana kuwa viongozi wametambua kweli kwamba huyu ndiye Kristo?
27 Kristo atakapokuja hakuna mtu atakayejua mahali alikotoka, lakini sisi
tunajua alikotoka mtu huyu!"
28 Basi, Yesu alipokuwa anafundisha Hekaluni alipaaza sauti na kusema,
"Ati mnanijua; hata nilikotoka mnakujua! Hata hivyo, sikuja kwa mamlaka
yangu mwenyewe; ila yeye aliyenituma mimi ni wa kweli, nanyi hamumjui.
29 Lakini mimi namjua kwa sababu nimetoka kwake, naye ndiye aliyenituma."
30 Basi, watu wakataka kumtia nguvuni, lakini hakuna mtu aliyethubutu kumkamata
kwa sababu saa yake ilikuwa haijafika bado.
31 Wengi katika ule umati wa watu walimwamini, wakasema,
"Je, Kristo akija atafanya ishara kubwa zaidi kuliko alizozifanya
huyu?"
32 Mafarisayo waliwasikia watu wakinong'ona maneno hayo juu ya Yesu. Basi,
wao pamoja na makuhani wakuu wakawatuma walinzi wamtie nguvuni.
33 Yesu akasema, "Bado niko nanyi kwa muda mfupi, kisha nitamwendea
yule aliyenituma.
34 Mtanitafuta lakini hamtaniona, maana pale nitakapokuwa ninyi hamwezi
kufika."
35 Viongozi wa Wayahudi wakasema wao kwa wao, "Mtu huyu atakwenda
wapi ambapo hatutaweza kumpata? Atakwenda kwa Wayahudi waliotawanyika kati
ya Wagiriki, na kuwafundisha Wagiriki?
36 Ana maana gani anaposema: <Mtanitafuta lakini hamtanipata, na mahali
nitakapokuwa ninyi hamwezi kufika?">
37 Siku ya mwisho ya sikukuu hiyo ilikuwa siku maalum. Yesu alisimama,
akasema kwa sauti kubwa, "Aliye na kiu na aje kwangu anywe.
38 Kama yasemavyo Maandiko Matakatifu: <Anayeniamini mimi, mito ya maji
yenye uzima itatiririka kutoka moyoni mwake!">
39 (Alisema hayo kumhusu Roho ambaye wale waliomwamini yeye watampokea.
Wakati huo Roho alikuwa hajafika kwa sababu Yesu alikuwa hajatukuzwa bado.)
40 Baadhi ya watu katika ule umati walisikia maneno hayo, wakasema, "Kweli
mtu huyu ndiye yule nabii!"
41 Wengine wakasema, "Huyu ndiye Kristo!" Lakini wengine walisema,
"Je, yawezekana Kristo akatoka Galilaya?
42 Maandiko Matakatifu yasemaje? Yanasema: <Kristo atatoka katika ukoo
wa Daudi, na atazaliwa Bethlehemu, mji wa Daudi!">
43 Basi, kukatokea mafarakano juu yake katika ule umati wa watu.
44 Baadhi ya watu walitaka kumtia nguvuni lakini hakuna aliyejaribu kumkamata.
45 Kisha wale walinzi wakarudi kwa makuhani wakuu na Mafarisayo; nao wakawauliza,
"Kwa nini hamkumleta?"
46 Walinzi wakawajibu, "Hakuna mtu aliyepata kamwe kusema kama asemavyo
mtu huyu!"
47 Mafarisayo wakawauliza, "Je, nanyi pia mmedanganyika?
48 Je, mmekwisha mwona hata mmoja wa viongozi wa watu, au mmoja wa Mafarisayo
aliyemwamini?
49 Lakini umati huu haujui Sheria ya Mose; umelaaniwa!"
50 Mmoja wao alikuwa Nikodemo ambaye hapo awali alikuwa amemwendea Yesu.
Basi, yeye akawaambia,
51 "Je, Sheria yetu humhukumu mtu kabla ya kumsikia kwanza na kujua
anafanya nini?"
52 Nao wakamjibu, "Je, wewe pia umetoka Galilaya? Haya, kayachunguze
Maandiko Matakatifu nawe utaona kwamba Galilaya hakutoki kamwe nabii!"
53 Basi, wote wakaondoka, kila mtu akaenda zake;
go to chapters........1-7.......8-14.......15-18.......19-21