John 8

 

 

 

1 lakini Yesu akaenda kwenye mlima wa Mizeituni.
2 Kesho yake asubuhi na mapema alikwenda tena Hekaluni. Watu wote wakamwendea, naye akaketi akawa anawafundisha.
3 Basi, walimu wa Sheria na Mafarisayo wakamletea mwanamke mmoja aliyefumaniwa katika uzinzi. Wakamsimamisha katikati yao.
4 Kisha wakamwuliza Yesu, "Mwalimu! Mwanamke huyu alifumaniwa katika uzinzi.
5 Katika Sheria yetu Mose alituamuru mwanamke kama huyu apigwe mawe. Basi, wewe wasemaje?"
6 Walisema hivyo kumjaribu, wapate kisa cha kumshtaki. Lakini Yesu akainama chini, akaandika ardhini kwa kidole.

7 Walipozidi kumwuliza, Yesu akainuka, akawaambia, "Mtu asiye na dhambi miongoni mwenu na awe wa kwanza kumpiga jiwe."
8 Kisha akainama tena, akawa anaandika ardhini.


9 Waliposikia hivyo, wakaanza kutoweka mmojammoja, wakitanguliwa na wazee. Yesu akabaki peke yake, na yule mwanamke amesimama palepale.
10 Yesu alipoinuka akamwuliza huyo mwanamke, "Wako wapi wale watu? Je, hakuna hata mmoja aliyekuhukumu?"


11 Huyo mwanamke akamjibu, "Mheshimiwa, hakuna hata mmoja!" Naye Yesu akamwambia, "Wala mimi sikuhukumu. Nenda zako; na tangu sasa usitende dhambi tena."
12 Yesu alipozungumza nao tena, aliwaambia, "Mimi ndimi mwanga wa ulimwengu. Anayenifuata mimi hatembei kamwe gizani, bali atakuwa na mwanga wa uzima."
13 Basi, Mafarisayo wakamwambia, "Wewe unajishuhudia mwenyewe; kwa hiyo ushahidi wako si halali."
14 Yesu akawajibu, "Hata kama ninajishuhudia mwenyewe, ushahidi wangu ni wa kweli kwa sababu mimi najua nilikotoka na ninakokwenda. Lakini ninyi hamjui nilikotoka wala ninakokwenda.
15 Ninyi mnahukumu kwa fikira za kibinadamu, lakini mimi simhukumu mtu.
16 Hata nikihukumu, hukumu yangu ni ya haki kwa sababu mimi siko peke yangu; Baba aliyenituma yuko pamoja nami.
17 Imeandikwa katika Sheria yenu ya kwamba ushahidi wa watu wawili ni halali.
18 Mimi najishuhudia mwenyewe, naye Baba aliyenituma, ananishuhudia pia."
19 Hapo wakamwuliza, "Baba yako yuko wapi?" Yesu akawajibu "Ninyi hamnijui mimi wala hamumjui Baba. Kama mngenijua mimi, mngemjua na Baba yangu pia."
20 Yesu alisema maneno hayo kwenye chumba cha hazina alipokuwa anafundisha Hekaluni. Wala hakuna mtu aliyemtia nguvuni, kwa sababu saa yake ilikuwa haijafika bado.
21 Yesu akawaambia tena, "Naenda zangu nanyi mtanitafuta, lakini mtakufa katika dhambi zenu. Niendako mimi, ninyi hamwezi kufika."
22 Basi, viongozi wa Wayahudi wakasema, "Je, atajiua? Mbona anasema: <Niendako ninyi hamwezi kufika?">
23 Yesu akawaambia, "Ninyi mmetoka papa hapa chini, mimi nimetoka juu; ninyi ni wa ulimwengu huu, mimi si wa ulimwengu huu.
24 Ndiyo maana niliwaambieni mtakufa katika dhambi zenu. Kama msipoamini kwamba <Mimi ndimi>, mtakufa katika dhambi zenu."
25 Nao wakamwuliza, "Wewe ni nani?" Yesu akawajibu, "Nimewaambieni tangu mwanzo!
26 Ninayo mengi ya kusema na kuhukumu juu yenu. Lakini yule aliyenituma ni kweli; nami nauambia ulimwengu mambo yale tu niliyoyasikia kutoka kwake."
27 Hawakuelewa kwamba Yesu alikuwa akisema nao juu ya Baba.
28 Basi, Yesu akawaambia, "Mtakapokwisha mwinua Mwana wa Mtu hapo ndipo mtakapojua kwamba <Mimi ndimi>, na kwamba sifanyi chochote mimi mwenyewe, ila nasema tu yale Baba aliyonifundisha.
29 Yule aliyenituma yuko pamoja nami; yeye hakuniacha peke yangu kwani nafanya daima yale yanayompendeza."
30 Baada ya kusema hayo watu wengi walimwamini.
31 Basi, Yesu akawaambia wale Wayahudi waliomwamini, "Kama mkiyazingatia mafundisho yangu mtakuwa kweli wanafunzi wangu.
32 Mtaujua ukweli, nao ukweli utawapeni uhuru."
33 Nao wakamjibu, "Sisi ni wazawa wa Abrahamu, na hatujapata kamwe kuwa watumwa wa mtu yeyote yule. Una maana gani unaposema: <mtakuwa huru?">
34 Yesu akawajibu, "Kweli nawaambieni, kila mtu anayetenda dhambi ni mtumwa wa dhambi.
35 Mtumwa hana makao ya kudumu nyumbani, lakini mwana anayo makao ya kudumu.
36 Kama mwana akiwapeni uhuru mtakuwa huru kweli.
37 Najua kwamba ninyi ni wazawa wa Abrahamu. Hata hivyo, mnataka kuniua kwa sababu hamuyakubali mafundisho yangu.
38 Mimi nasema yale aliyonionyesha Baba, lakini ninyi mwafanya yale aliyowaambieni baba yenu."
39 Wao wakamjibu, "Baba yetu ni Abrahamu!" Yesu akawaambia, "Kama ninyi mngekuwa watoto wa Abrahamu, mngefanya kama alivyofanya Abrahamu,
40 Mimi nimewaambieni ukweli niliousikia kwa Mungu; hata hivyo, ninyi mwataka kuniua. Abrahamu hakufanya hivyo!
41 Ninyi mnafanya mambo yaleyale aliyofanya babu yenu." Wao wakamwambia, "Sisi si watoto haramu! Tunaye baba mmoja tu, yaani Mungu."
42 Yesu akawaambia, "Kama Mungu angekuwa Baba yenu, mngenipenda mimi, maana mimi nilitoka kwa Mungu na sasa niko hapa. Sikuja kwa mamlaka yangu mwenyewe, ila yeye alinituma.
43 Kwa nini hamwelewi hayo ninayosema? Ni kwa kuwa hamwezi kuusikiliza ujumbe wangu.
44 Ninyi ni watoto wa baba yenu Ibilisi na mnataka tu kutekeleza tamaa za baba yenu. Yeye alikuwa muuaji tangu mwanzo; hana msimamo katika ukweli, kwani ukweli haumo ndani yake. Kila asemapo uongo, husema kutokana na hali yake ya maumbile, maana yeye ni mwongo na baba wa uongo.
45 Mimi nasema ukweli, na ndiyo maana ninyi hamniamini.
46 Nani kati yenu awezaye kuthibitisha kuwa mimi nina dhambi? Ikiwa basi nasema ukweli, kwa nini hamniamini?
47 Aliye wa Mungu husikiliza maneno ya Mungu. Lakini ninyi hamsikilizi kwa sababu ninyi si (watu wa) Mungu."
48 Wayahudi wakamwambia, "Je, hatukusema kweli kwamba wewe ni Msamaria, na tena una pepo?"
49 Yesu akajibu, "Mimi sina pepo; mimi namheshimu Baba yangu, lakini ninyi hamniheshimu.
50 Mimi sijitafutii utukufu wangu mwenyewe; yuko mmoja mwenye kuutafuta utukufu huo, naye ni hakimu.
51 Kweli nawaambieni, anayeuzingatia ujumbe wangu hatakufa milele."
52 Basi, Wayahudi wakasema, "Sasa tunajua kweli kwamba wewe ni mwendawazimu! Abrahamu alikufa, na manabii pia walikufa, nawe wasema ati, <Anayeuzingatia ujumbe wangu hatakufa milele!>
53 Je, unajifanya mkuu zaidi kuliko baba yetu Abrahamu ambaye alikufa? Hata na manabii walikufa. Wewe unajifanya kuwa nani?"
54 Yesu akawajibu, "Nikijitukuza mwenyewe, utukufu wangu si kitu. Baba yangu ambaye ninyi mwasema ni Baba yenu, ndiye anayenitukuza.
55 Ninyi hamjapata kumjua, lakini mimi namjua. Na, nikisema simjui, nitakuwa mwongo kama ninyi. Mimi namjua na ninashika neno lake.
56 Abrahamu, baba yenu, alishangilia aione siku yangu; naye aliiona, akafurahi."
57 Basi, Wayahudi wakamwambia, "Wewe hujatimiza miaka hamsini bado, nawe umemwona Abrahamu?"
58 Yesu akawaambia, "Kweli nawaambieni, kabla Abrahamu hajazaliwa, mimi niko."
59 Hapo wakaokota mawe ili wamtupie, lakini Yesu akajificha, akatoka Hekaluni.


John 9

 

 

1 Yesu alipokuwa akipita alimwona mtu mmoja, kipofu tangu kuzaliwa.
2 Basi, wanafunzi wakamwuliza, "Mwalimu! Ni nani aliyetenda dhambi: mtu huyu, ama wazazi wake, hata akazaliwa kipofu?"
3 Yesu akajibu, "Jambo hili halikutukia kwa sababu ya dhambi zake yeye, wala dhambi za wazazi wake; ila alizaliwa kipofu ili nguvu ya Mungu ionekane ikifanya kazi ndani yake.
4 Kukiwa bado mchana yatupasa kuendelea kufanya kazi za yule aliyenituma; maana usiku unakuja ambapo mtu hawezi kufanya kazi.
5 Wakati ningali ulimwenguni, mimi ni mwanga wa ulimwengu."
6 Baada ya kusema hayo, akatema mate chini, akafanyiza tope, akampaka yule kipofu machoni,


7 akamwambia, "Nenda ukanawe katika bwawa la Siloamu." (maana ya jina hili ni "aliyetumwa"). Basi, huyo kipofu akaenda, akanawa, kisha akarudi akiwa anaona.
8 Basi, jirani zake na wale waliokuwa wanajua kwamba hapo awali alikuwa maskini mwombaji, wakasema, "Je, huyu siye yule maskini aliyekuwa akiketi na kuomba?"


9 Baadhi yao wakasema, "Ndiye." Wengine wakasema, "La! Ila anafanana naye." Lakini huyo aliyekuwa kipofu akasema, "Ni mimi!"
10 Basi, wakamwuliza, "Sasa, macho yako yalipataje kufumbuliwa?"
11 Naye akawajibu, "Yule mtu aitwaye Yesu alifanya tope, akanipaka machoni na kuniambia: <Nenda ukanawe katika bwawa la Siloamu.> Basi, mimi nikaenda, nikanawa, nikapata kuona."
12 Wakamwuliza, "Yeye yuko wapi?" Naye akawajibu, "Mimi sijui!"
13 Kisha wakampeleka huyo mtu aliyekuwa kipofu kwa Mafarisayo.
14 Siku hiyo Yesu alipofanya tope na kumfumbua macho mtu huyo, ilikuwa siku ya Sabato.
15 Basi, Mafarisayo wakamwuliza mtu huyo, "Umepataje kuona?" Naye akawaambia, "Alinipaka tope machoni, nami nikanawa na sasa naona."
16 Baadhi ya Mafarisayo wakasema, "Mtu huyu hakutoka kwa Mungu, maana hashiki sheria ya Sabato." Lakini wengine wakasema, "Mtu mwenye dhambi awezaje kufanya ishara za namna hii?" Kukawa na mafarakano kati yao.
17 Wakamwuliza tena huyo mtu aliyekuwa kipofu, "Maadam yeye amekufungua macho, wasemaje juu yake?" Naye akawaambia, "Yeye ni nabii!"
18 Viongozi wa Wayahudi hawakusadiki kwamba mtu huyo alikuwa kipofu hapo awali na sasa anaona mpaka walipowaita wazazi wake.
19 Basi, wakawauliza hao wazazi, "Je, huyu ndiye mtoto wenu ambaye ninyi mwasema alizaliwa kipofu? Sasa amepataje kuona?"
20 Wazazi wake wakajibu, "Tunajua kwamba huyu ni mtoto wetu, na kwamba alizaliwa kipofu.
21 Lakini amepataje kuona, hatujui; na wala hatumjui yule aliyemfumbua macho. Mwulizeni yeye mwenyewe; yeye ni mtu mzima, anaweza kujitetea mwenyewe."
22 Wazazi wake walisema hivyo kwa sababu waliwaogopa viongozi wa Wayahudi kwani viongozi hao walikuwa wamepatana ya kwamba mtu yeyote atakayekiri kwamba Yesu ni Kristo atafukuzwa nje ya sunagogi.
23 Ndiyo maana wazazi wake walisema: "Yeye ni mtu mzima, mwulizeni."
24 Basi, wakamwita tena aliyekuwa kipofu, wakamwambia, "Sema ukweli mbele ya Mungu! Sisi tunajua kwamba mtu huyu ni mwenye dhambi."
25 Yeye akajibu, "Kama ni mwenye dhambi mimi sijui. Lakini kitu kimoja najua: Nilikuwa kipofu, na sasa naona."
26 Basi, wakamwuliza, "Alikufanyia nini? Alikufumbuaje macho yako?"


27 Huyo mtu akawajibu, "Nimekwisha waambieni, nanyi hamkusikiliza; kwa nini mwataka kusikia tena? Je, ninyi pia mnataka kuwa wafuasi wake?"
28 Lakini wao wakamtukana wakisema, "Wewe ni mfuasi wake; sisi ni wafuasi wa Mose.
29 Sisi tunajua kwamba Mungu alisema na Mose, lakini mtu huyu hatujui ametoka wapi!"
30 Naye akawajibu, "Hili ni jambo la kushangaza! Ninyi hamjui ametoka wapi, lakini amenifumbua macho yangu!
31 Tunajua kwamba Mungu hawasikilizi watu wenye dhambi, ila humsikiliza yeyote mwenye kumcha na kutimiza mapenzi yake.
32 Tangu mwanzo wa ulimwengu haijasikika kwamba mtu ameyafumbua macho ya mtu aliyezaliwa kipofu.
33 Kama mtu huyu hakutoka kwa Mungu, hangeweza kufanya chochote!"
34 Wao wakamjibu, "Wewe ulizaliwa na kulelewa katika dhambi; unawezaje kutufundisha sisi?" Basi, wakamfukuzia mbali.
35 Yesu alisikia kwamba walikuwa wamemfukuzia mbali, naye alipomkuta akamwuliza, "Je, wewe unamwamini Mwana wa Mtu?"
36 Huyo mtu akajibu, "Mheshimiwa, niambie yeye ni nani, ili nipate kumwamini."
37 Yesu akamwambia, "Umekwisha mwona, naye ndiye anayesema nawe sasa."


38 Basi, huyo mtu akasema, "Ninaamini Bwana!" Akamsujudia.
39 Yesu akasema, "Mimi nimekuja ulimwenguni kutoa hukumu, kusudi wasioona wapate kuona, na wale wanaoona wawe vipofu."
40 Baadhi ya Mafarisayo waliokuwa pamoja naye walisikia maneno hayo, wakamwuliza, "Je, sisi pia ni vipofu?"
41 Yesu akawajibu, "Kama mngekuwa vipofu, hamngekuwa na hatia; lakini sasa ninyi mwasema: <Sisi tunaona>, na hiyo yaonyesha kwamba mna hatia bado.

 

John 10

 

 

1 Yesu alisema "Kweli nawaambieni, yeyote yule asiyeingia katika zizi la kondoo kwa kupitia mlangoni, bali hupenya na kuingia kwa njia nyingine, huyo ni mwizi na mnyang'anyi.
2 Lakini anayeingia kwa kupitia mlangoni, huyo ndiye mchungaji wa kondoo.
3 Mngoja mlango wa zizi humfungulia, na kondoo husikia sauti yake, naye huwaita kondoo wake kila mmoja kwa jina lake na kuwaongoza nje.
4 Akisha watoa nje huwatangulia mbele nao kondoo humfuata, kwani wanaijua sauti yake.
5 Kondoo hao hawawezi kumfuata mgeni, bali watamkimbia kwa sababu hawaijui sauti yake."
6 Yesu aliwaambia mfano huo, lakini wao hawakuelewa alichotaka kuwaambia.
7 Basi, akasema tena, "Kweli nawaambieni, mimi ni mlango wa kondoo.
8 Wale wengine wote waliokuja kabla yangu ni wezi na wanyang'anyi, nao kondoo hawakuwasikiliza.
9 Mimi ni mlango. Anayeingia kwa kupitia kwangu ataokolewa; ataingia na kutoka, na kupata malisho.
10 Mwizi huja kwa shabaha ya kuiba, kuua na kuharibu. Mimi nimekuja mpate kuwa na uzima--uzima kamili.
11 "Mimi ni mchungaji mwema. Mchungaji mwema huutoa uhai wake kwa ajili ya kondoo wake.
12 Mtu wa kuajiriwa ambaye si mchungaji, na wala kondoo si mali yake, anapoona mbwa mwitu anakuja, huwaacha kondoo na kukimbia. Kisha mbwa mwitu huwakamata na kuwatawanya.
13 Yeye hajali kitu juu ya kondoo kwa sababu yeye ni mtu wa mshahara tu.
14 Mimi ni mchungaji mwema. Nawajua walio wangu, nao walio wangu wananijua mimi,
15 kama vile Baba anijuavyo, nami nimjuavyo Baba. Mimi nayatoa maisha yangu kwa ajili yao.
16 Tena ninao kondoo wengine ambao hawamo zizini humu. Inanibidi kuwaleta hao pia, nao wataisikia sauti yangu, na kutakuwako kundi moja na mchungaji mmoja.
17 "Baba ananipenda kwani nautoa uhai wangu ili nipate kuupokea tena.
18 Hakuna mtu anayeninyang'anya uhai wangu; mimi na nautoa kwa hiari yangu mwenyewe. Ninao uwezo wa kuutoa na uwezo wa kuuchukua tena. Hivi ndivyo Baba alivyoniamuru nifanye."
19 Kukawa tena na mafarakano kati ya Wayahudi kwa sababu ya maneno haya.
20 Wengi wao wakasema, "Ana pepo; tena ni mwendawazimu! Ya nini kumsikiliza?"
21 Wengine wakasema, "Haya si maneno ya mwenye pepo. Je, pepo anaweza kuyafumbua macho ya vipofu?"
22 Huko Yerusalemu kulikuwa na sikukuu ya Kutabaruku. Wakati huo ulikuwa wa baridi.
23 Naye Yesu akawa anatembea Hekaluni katika ukumbi wa Solomoni.
24 Basi, Wayahudi wakamzunguka, wakamwuliza, "Utatuacha katika mashaka mpaka lini? Kama wewe ndiye Kristo, basi, tuambie wazi."


25 Yesu akawajibu, "Nimewaambieni, lakini hamsadiki. Kazi ninazozifanya mimi kwa jina la Baba yangu zinanishuhudia.
26 Lakini ninyi hamsadiki kwa sababu ninyi si kondoo wangu.
27 Kondoo wangu huisikia sauti yangu; mimi nawajua, nao hunifuata.
28 Mimi nawapa uzima wa milele; nao hawatapotea milele, wala hakuna mtu atakayeweza kuwatoa mkononi mwangu.
29 Baba yangu ambaye ndiye aliyenipa hao ni mkuu kuliko wote, wale hakuna awezaye kuwatoa mikononi mwake Baba.
30 Mimi na Baba, tu mmoja."
31 Basi, Wayahudi wakachukua mawe ili wamtupie.
32 Yesu akawaambia, "Nimewaonyesheni kazi nyingi kutoka kwa Baba. Ni ipi kati ya hizo inayowafanya mnipige mawe?"


33 Wayahudi wakamjibu, "Hatukupigi mawe kwa ajili ya tendo jema, ila kwa sababu ya kukufuru! Maana wajifanya kuwa Mungu hali wewe ni binadamu tu."
34 Yesu akawajibu, "Je, haikuandikwa katika Sheria yenu: <Mimi nimesema, ninyi ni miungu?>
35 Mungu aliwaita miungu wale waliopewa neno lake; nasi twajua kwamba Maandiko Matakatifu yasema ukweli daima.
36 Je, yeye ambaye Baba alimweka wakfu na kumtuma ulimwenguni, mnamwambia: <Unakufuru>, eti kwa sababu nilisema: <Mimi ni Mwana wa Mungu?>
37 Kama sifanyi kazi za Baba yangu msiniamini.
38 Lakini ikiwa ninazifanya, hata kama hamniamini, walau ziaminini hizo kazi mpate kujua na kutambua kwamba Baba yuko ndani yangu, nami niko ndani yake."
39 Wakajaribu tena kumkamata lakini akachopoka mikononi mwao.
40 Yesu akaenda tena ng'ambo ya mto Yordani, mahali Yohane alipokuwa akibatiza, akakaa huko.
41 Watu wengi walimwendea wakasema, "Yohane hakufanya ishara yoyote. Lakini yale yote Yohane aliyosema juu ya mtu huyu ni kweli kabisa."
42 Watu wengi mahali hapo wakamwamini.

 

John 11

 

1 Mtu mmoja aitwaye Lazaro, mwenyeji wa Bethania, alikuwa mgonjwa. (Kijiji cha Bethania kilikuwa mahali walipokaa Maria na Martha, dada yake.
2 Maria ndiye yule aliyempaka Bwana marashi na kumpangusa kwa nywele zake. Lazaro, kaka yake, ndiye aliyekuwa mgonjwa.)
3 Basi, hao dada wakatuma ujumbe huu kwa Yesu: "Bwana, rafiki yako ni mgonjwa!"
4 Yesu aliposikia hivyo akasema, "Ugonjwa huo hautaleta kifo, ila ni kwa ajili ya kumtukuza Mungu; ameugua ili kwa njia hiyo Mwana wa Mungu atukuzwe."
5 Yesu aliwapenda Martha, dada yake na Lazaro.
6 Alipopata habari kwamba Lazaro ni mgonjwa, Yesu aliendelea kukaa mahali hapo alipokuwa kwa siku mbili zaidi.
7 Kisha akawaambia wanafunzi wake, "Twendeni tena Yudea!"
8 Wanafunzi wakamwambia, "Mwalimu! Muda mfupi tu umepita tangu Wayahudi walipotaka kukuua kwa mawe, nawe unataka kwenda huko tena?"
9 Yesu akajibu, "Je, saa za mchana si kumi na mbili? Basi, mtu akitembea mchana hawezi kujikwaa kwa kuwa anauona mwanga wa ulimwengu huu.
10 Lakini mtu akitembea usiku atajikwaa kwa maana mwanga haumo ndani yake."
11 Yesu alipomaliza kusema maneno hayo, akawaambia, "Rafiki yetu Lazaro amelala, lakini mimi nitakwenda kumwamsha."
12 Wanafunzi wake wakamwambia, "Bwana, ikiwa amelala, basi atapona."
13 Wao walidhani kwamba alikuwa amesema juu ya kulala usingizi, kumbe alikuwa amesema juu ya kifo cha Lazaro.
14 Basi, Yesu akawaambia waziwazi, "Lazaro amekufa;
15 Lakini nafurahi kwa ajili yenu kwamba sikuwako huko, ili mpate kuamini. Haya, twendeni kwake."
16 Thoma (aitwaye Pacha) akawaambia wanafunzi wenzake, "Twendeni nasi tukafe pamoja naye!"
17 Yesu alipofika huko alikuta Lazaro amekwisha kaa kaburini kwa siku nne.
18 Kijiji cha Bethania kilikuwa karibu na Yerusalemu umbali upatao kilomita tatu.
19 Wayahudi wengi walikuwa wamefika kwa Martha na Maria kuwafariji kwa kifo cha kaka yao.
20 Basi, Martha aliposikia kwamba Yesu alikuwa anakuja, akaenda kumlaki; lakini Maria alibaki nyumbani.
21 Martha akamwambia Yesu, "Bwana, kama ungalikuwa hapa, kaka yangu hangalikufa!
22 Lakini najua kwamba hata sasa chochote utakachomwomba Mungu, atakupa."
23 Yesu akamwambia, "Kaka yako atafufuka."
24 Martha akamjibu, "Najua kwamba atafufuka wakati wa ufufuo, siku ya mwisho."
25 Yesu akamwambia, "Mimi ndimi ufufuo na uzima. Anayeniamini mimi hata kama anakufa, ataishi:
26 na kila anayeishi na kuniamini, hatakufa kamwe. Je, waamini hayo?"
27 Martha akamwambia, "Ndiyo Bwana! Naamini kwamba wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu, yule ajaye ulimwenguni."
28 Baada ya kusema hayo, Martha alikwenda kumwita Maria, dada yake, akamwabia faraghani, "Mwalimu yuko hapa, anakuita."


29 Naye aliposikia hivyo, akainuka mara, akamwendea Yesu.
30 Yesu alikuwa hajaingia kijijini, ila alikuwa bado mahali palepale Martha alipomlaki.
31 Basi, Wayahudi waliokuwa nyumbani pamoja na Maria wakimfariji walipomwona ameinuka na kutoka nje ghafla, walimfuata. Walidhani alikuwa anakwenda kaburini kuomboleza.
32 Basi, Maria alipofika mahali pale Yesu alipokuwa na kumwona, alipiga magoti, akamwabia, "Bwana, kama ungalikuwa hapa, kaka yangu hangalikufa!"


33 Yesu alipomwona analia, na wale Wayahudi waliokuja pamoja naye wanalia pia, alijawa na huzuni na kufadhaika moyoni.
34 Kisha akawauliza, "Mlimweka wapi?" Wakamwambia, "Bwana, njoo uone."
35 Yesu akalia machozi.
36 Basi, Wayahudi wakasema, "Tazameni jinsi alivyompenda!"
37 Lakini baadhi yao wakasema, "Je, huyu aliyemfumbua macho yule kipofu, hakuweza kumfanya Lazaro asife?"
38 Basi, Yesu akiwa amehuzunika tena moyoni, akafika kaburini. Kaburi lenyewe lilikuwa pango, na lilikuwa limefunikwa kwa jiwe.
39 Yesu akasema, "Ondoeni hilo jiwe!" Martha, dada yake huyo aliyekufa, akamwambia, "Bwana, amekwishaanza kunuka; amekaa kaburini siku nne!"
40 Yesu akamwambia, "Je, sikukwambia kwamba ukiamini utaona utukufu wa Mungu?"
41 Basi, wakaliondoa lile jiwe. Yesu akatazama juu mbinguni, akasema, "Nakushukuru Baba kwa kuwa wewe wanisikiliza.
42 Najua kwamba unanisikiliza daima. Lakini nimesema hayo kwa ajili ya watu hawa waliopo hapa ili wapate kuamini kwamba wewe ndiwe uliyenituma."
43 Alipokwisha sema hayo, akaita kwa sauti kubwa: "Lazaro! Toka nje!"
44 Huyo aliyekuwa amekufa akatoka nje, huku amefungwa sanda miguu na mikono, na uso wake umefunikwa. Yesu akawaambia, "Mfungueni, mkamwache aende zake."
45 Basi, Wayahudi wengi waliokuwa wamefika kwa Maria walipoona kitendo hicho alichokifanya Yesu wakamwamini.
46 Lakini baadhi yao walikwenda kwa Mafarisayo wakatoa taarifa ya jambo hilo alilofanya Yesu.


47 kwa hiyo makuhani wakuu na Mafarisayo wakafanya kikao cha Baraza kuu, wakasema, "Tufanye nini? Mtu huyu anafanya ishara nyingi mno.
48 Tukimwacha tu watu wote watamwamini, nao Waroma watakuja kuliharibu Hekalu letu na taifa letu!"
49 Hapo, mmoja wao aitwaye Kayafa, ambaye alikuwa Kuhani Mkuu mwaka huo, akawaambia, "Ninyi hamjui kitu!
50 Je, hamwoni kwamba ni afadhali kwenu mtu mmoja afe kwa ajili ya watu, kuliko taifa zima liangamizwe?"
51 Yeye hakusema hivyo kwa hiari yake mwenyewe, bali kwa vile alikuwa Kuhani Mkuu mwaka huo, alibashiri kwamba Yesu atakufa kwa ajili ya taifa lao;
52 na wala si kwa ajili yao tu, bali pia apate kuwaleta pamoja watoto wa Mungu waliotawanyika.
53 Basi, tangu siku hiyo viongozi wa Wayahudi walifanya mipango ya kumwua Yesu.
54 Kwa hiyo, Yesu hakutembea tena hadharani kati ya Wayahudi, bali alitoka hapo, akaenda mahali karibu na jangwa, katika mji uitwao Efraimu. Akakaa huko pamoja na wanafunzi wake.
55 Sikukuu ya Wayahudi ya Pasaka ilikuwa karibu, na watu wengi walikwenda Yerusalemu ili wajitakase kabla ya sikukuu hiyo.
56 Basi, wakawa wanamtafuta Yesu; nao walipokusanyika pamoja Hekaluni wakaulizana, "Mwaonaje? Yaonekana kwamba haji kabisa kwenye sikukuu, au sivyo?"
57 Makuhani wakuu na Mafarisayo walikuwa wametoa amri kwamba mtu akijua mahali aliko Yesu awaarifu kusudi wamtie nguvuni.

 

John 12

 

 

 

 

1 Siku sita kabla ya sikukuu ya Pasaka, Yesu alifika Bethania alikoishi Lazaro ambaye Yesu alikuwa amemfufua kutoka wafu.
2 Huko walimwandalia chakula cha jioni, naye Martha akawa anawatumikia. Lazaro alikuwa mmoja wa wale waliokuwa mezani pamoja na Yesu.
3 Basi, Maria alichukua chupa ya marashi ya nardo safi ya thamani kubwa, akampaka Yesu miguu na kuipangusa kwa nywele zake. Nyumba yote ikajaa harufu ya marashi.
4 Basi, Yuda Iskarioti, mmoja wa wale kumi na wawili ambaye ndiye atakayemsaliti Yesu, akasema,
5 "Kwa nini marashi hayo hayakuuzwa kwa fedha dinari mia tatu, wakapewa maskini?"
6 Alisema hivyo, si kwa kuwa alijali chochote juu ya maskini, bali kwa sababu alikuwa mweka hazina, na kwa kuwa alikuwa mwizi, mara kwa mara aliiba kutoka katika hiyo hazina.
7 Lakini Yesu akasema, "Msimsumbue huyu mama! Mwacheni ayaweke kwa ajili ya siku ya mazishi yangu.
8 Maskini mtakuwa nao siku zote, lakini hamtakuwa nami siku zote."
9 Wayahudi wengi walisikia kwamba Yesu alikuwa Bethania. Basi, wakafika huko si tu kwa ajili ya kumwona Yesu, ila pia wapate kumwona Lazaro ambaye Yesu alimfufua kutoka wafu.
10 Makuhani wakuu waliamua pia kumwua Lazaro,
11 Maana kwa sababu ya Lazaro Wayahudi wengi waliwaasi viongozi wao, wakamwamini Yesu.
12 Kesho yake, kundi kubwa la watu waliokuja kwenye sikukuu walisikia kuwa Yesu alikuwa njiani kuja Yerusalemu.
13 Basi, wakachukua matawi ya mitende, wakatoka kwenda kumlaki; wakapaaza sauti wakisema: "Hosana! Abarikiwe huyo ajaye kwa jina la Bwana. Abarikiwe mfalme wa Israeli."
14 Yesu akampata mwana punda mmoja akapanda juu yake kama yasemavyo Maandiko:
15 "Usiogope mji wa Sioni! Tazama, Mfalme wako anakuja, Amepanda mwana punda."
16 Wakati huo wanafunzi wake hawakuelewa mambo hayo, lakini Yesu alipokwisha tukuzwa, ndipo walipokumbuka kwamba hayo yalikuwa yameandikwa juu yake, na kwamba watu walikuwa wamemtendea hivyo.
17 Kundi la watu wale waliokuwa pamoja naye wakati alipomwita Lazaro kutoka kaburini, akamfufua kutoka wafu, walisema yaliyotukia.
18 Kwa hiyo umati huo wa watu ulimlaki, maana wote walisikia kwamba Yesu alikuwa amefanya ishara hiyo.
19 Basi, Mafarisayo wakaambiana, "Mnaona? Hatuwezi kufanya chochote! Tazameni, ulimwengu wote unamfuata."
20 Kulikuwa na Wagiriki kadhaa miongoni mwa watu waliokuwa wamefika Yerusalemu kuabudu wakati wa sikukuu hiyo.
21 Hao walimwendea Filipo, mwenyeji wa Bethsaida katika Galilaya, wakasema, "Mheshimiwa, tunataka kumwona Yesu."
22 Filipo akaenda akamwambia Andrea, nao wawili wakaenda kumwambia Yesu.
23 Yesu akawaambia, "Saa ya kutukuzwa kwa Mwana wa Mtu imefika!
24 Kweli nawaambieni, punje ya ngano hubaki punje tu isipokuwa ikianguka katika udongo na kufa. Kama ikifa, basi huzaa matunda mengi.
25 Anayependa maisha yake, atayapoteza; anayeyachukia maisha yake katika ulimwengu huu, atayaweka kwa ajili ya uzima wa milele.
26 Anayetaka kunitumikia ni lazima anifuate, hivyo kwamba popote pale nilipo mimi ndipo na mtumishi wangu atakapokuwa. Mtu yeyote anayenitumikia Baba yangu atampa heshima.
27 "Sasa roho yangu imefadhaika, na niseme nini? Je, niseme: <Baba, usiruhusu saa hii inifikie>? Lakini ndiyo maana nimekuja--ili nipite katika saa hii.
28 Baba, ulitukuze jina lako." Hapo sauti ikasema kutoka mbinguni, "Nimelitukuza, na nitalitukuza tena."


29 Umati wa watu waliokuwa wamesimama hapo walisikia sauti hiyo, na baadhi yao walisema, "Malaika ameongea naye!"
30 Lakini Yesu akawaambia, "Sauti hiyo haikutokea kwa ajili yangu mimi, ila kwa ajili yenu.
31 Sasa ndio wakati wa ulimwengu huu kuhukumiwa; sasa mtawala wa ulimwengu huu atapinduliwa.
32 Nami nitakapoinuliwa juu ya nchi nitamvuta kila mmoja kwangu."
33 (Kwa kusema hivyo alionyesha atakufa kifo gani).
34 Basi, umati huo ukamjibu, "Sisi tunaambiwa na Sheria yetu kwamba Kristo atadumu milele. Wawezaje basi, kusema ati Mwana wa Mtu anapaswa kuinuliwa? Huyo Mwana wa Mtu ni nani?"
35 Yesu akawaambia, "Mwanga bado uko nanyi kwa muda mfupi. Tembeeni mngali mnao huo mwanga ili giza lisiwapate; maana atembeaye gizani hajui aendako.
36 Basi, wakati mnao huo mwanga uaminini ili mpate kuwa watu wa mwanga." Baada ya kusema maneno hayo, Yesu alikwenda zake na kujificha mbali nao.
37 Ingawa Yesu alifanya miujiza hii yote mbele yao, wao hawakumwamini.


38 Hivyo maneno aliyosema nabii Isaya yakatimia: "Bwana, nani aliyeuamini ujumbe wetu? Na uwezo wa Bwana umedhihirishwa kwa nani?"
39 Hivyo hawakuweza kuamini, kwani Isaya tena alisema:
40 "Mungu ameyapofusha macho yao, amezipumbaza akili zao; wasione kwa macho yao, wasielewe kwa akili zao; wala wasinigeukie, asema Bwana, ili nipate kuwaponya."
41 Isaya alisema maneno haya kwa sababu aliuona utukufu wa Yesu, akasema habari zake.
42 Hata hivyo, wengi wa viongozi wa Wayahudi walimwamini Yesu. Lakini kwa sababu ya Mafarisayo, hawakumkiri hadharani kwa kuogopa kwamba watatengwa na sunagogi.
43 Walipendelea kusifiwa na watu kuliko kusifiwa na Mungu
44 Kisha Yesu akasema kwa sauti kubwa, "Mtu aliyeniamini, haniamini mimi tu, ila anamwamini pia yule aliyenituma.


45 Anayeniona mimi anamwona pia yule aliyenituma.
46 Mimi ni mwanga, nami nimekuja ulimwenguni ili wote wanaoniamini wasibaki gizani.
47 Anayeyasikia maneno yangu lakini hayashiki mimi sitamhukumu; maana sikuja kuhukumu ulimwengu bali kuuokoa.
48 Asiyeyashika maneno yangu anaye wa kumhukumu: neno lile nililosema ni hakimu wake siku ya mwisho.
49 Mimi sikunena kwa mamlaka yangu mwenyewe, ila Baba aliyenituma ndiye aliyeniamuru niseme nini na niongee nini.
50 Nami najua kuwa amri yake huleta uzima wa milele. Basi, mimi nasema tu yale Baba aliyoniagiza niyaseme."

 

John 13

 

 

 

1 Ilikuwa kabla ya sikukuu ya Pasaka. Yesu alijua kwamba saa yake ya kuondoka ulimwenguni na kwenda kwa Baba ilikuwa imefika. Alikuwa amewapenda daima watu wake walioko duniani; naam, aliwapenda mpaka mwisho!
2 Basi, Yesu na wanafunzi wake walikuwa mezani kwa chakula cha jioni. Ibilisi alikwisha mtia Yuda, mwana wa Simoni Iskarioti, nia ya kumsaliti Yesu.
3 Yesu alijua kwamba Baba alikuwa amemkabidhi kila kitu, na kwamba alikuwa ametoka kwa Mungu na anarudi kwa Mungu.
4 Basi, Yesu aliondoka mezani, akaweka kando vazi lake, akachukua kitambaa na kujifunga kiunoni.
5 Kisha akatia maji katika bakuli, akaanza kuwaosha wanafunzi wake miguu na kuipangusa kwa kile kitambaa alichojifungia.
6 Basi, akamfikia Simoni Petro; naye Petro akasema, "Bwana, wewe utaniosha miguu mimi?"
7 Yesu akamjibu, "Huelewi sasa ninachofanya lakini utaelewa baadaye."
8 Petro akamwambia, "Wewe hutaniosha miguu kamwe!" Yesu akamjibu, "Nisipokuosha hutakuwa na uhusiano nami tena."
9 Simoni Petro akamwambia, "Bwana, nioshe, si miguu tu, bali na mikono yangu na kichwa pia."


10 Yesu akamwambia, "Aliyekwisha oga hana lazima ya kunawa isipokuwa miguu, maana amekwisha takata mwili wote. Ninyi mmetakata, lakini si nyote."
11 (Yesu alimjua yule ambaye atamsaliti, ndiyo maana alisema: "Ninyi mmetakata, lakini si nyote.")
12 Alipokwisha waosha miguu na kuvaa tena vazi lake, aliketi mezani, akawaambia, "Je, mmeelewa hayo niliyowatendeeni?
13 Ninyi mwaniita Mwalimu na Bwana, nanyi mwasema vyema, kwa kuwa ndimi.
14 Basi, ikiwa mimi niliye Bwana na Mwalimu, nimewaosha ninyi miguu, nanyi pia mnapaswa kuoshana miguu.
15 Nimewapeni mfano, ili nanyi pia mfanye kama nilivyowafanyieni.
16 Kweli nawaambieni, mtumishi si mkuu zaidi kuliko bwana wake, wala mtume si mkuu zaidi kuliko yule aliyemtuma.
17 Basi, ikiwa mwayajua hayo, mtakuwa na heri mkiyatekeleza.
18 "Haya nisemayo hayawahusu ninyi nyote. Mimi nawajua wale niliowachagua. Lakini lazima yatimie Maandiko Matakatifu yasemayo: <Yule aliyeshiriki chakula changu amegeuka kunishambulia.>
19 Mimi nimewaambieni mambo haya sasa kabla hayajatokea, ili yatakapotokea mpate kuamini kuwa mimi ndimi.
20 Kweli nawaambieni anayempokea yule ninayemtuma anaponipokea mimi; na anayenipokea mimi, anampokea yule aliyenituma."
21 Alipokwisha sema hayo, Yesu alifadhaika sana rohoni, akasema wazi, "Kweli nawaambieni, mmoja wenu atanisaliti!"
22 Wanafunzi wakatazama wasiweze kabisa kujua anasema nani.
23 Mmoja wa wanafunzi, ambaye Yesu alikuwa anampenda sana, alikuwa ameketi karibu na Yesu.
24 Basi, Simoni Petro akamwashiria na kusema: "Mwulize anasema juu ya nani."
25 Mwanafunzi huyo akasogea karibu zaidi na Yesu, akamwuliza, "Bwana, ni nani?"
26 Yesu akajibu, "Yule nitakayempa kipande cha mkate nilichochovya katika sahani, ndiye." Basi, akatwaa kipande cha mkate, akakichovya katika sahani, akampa Yuda, mwana wa Simoni Iskarioti.
27 Yuda alipokwisha pokea kipande hicho, Shetani akamwingia. Basi Yesu akamwambia, "Unachotaka kufanya, kifanye haraka!"
28 Lakini hakuna hata mmoja wa wale waliokaa pale mezani aliyefahamu kwa nini alikuwa amemwambia hivyo.
29 Kwa kuwa Yuda alikuwa na wajibu wa kuutunza mfuko wa fedha, baadhi yao walidhani kwamba Yesu alikuwa amemwambia anunue vilivyohitajiwa kwa sikukuu, au kwamba alikuwa amemwambia akatoe chochote kwa maskini.
30 Basi, Yuda alipokwisha twaa kile kipande cha mkate, akatoka nje mara. Na ilikuwa usiku.
31 Baada ya Yuda kuondoka, Yesu akasema, "Sasa Mwana wa Mtu ametukuzwa, naye Mungu ametukuzwa ndani yake.
32 Na kama utukufu wa Mungu umefunuliwa ndani ya Mwana, basi, naye Mungu ataudhihirisha utukufu wa Mwana ndani yake mwenyewe, na atafanya hivyo mara.
33 "Watoto wangu, bado niko nanyi kwa muda mfupi tu. Mtanitafuta, lakini sasa nawaambieni yale niliyowaambia viongozi wa Wayahudi: <Niendako ninyi hamwezi kwenda!>
34 Nawapeni amri mpya: pendaneni; pendaneni kama nilivyowapenda ninyi.
35 Mkipendana, watu wote watajua kwamba ninyi ni wanafunzi wangu."
36 Simoni Petro akamwuliza, "Bwana, unakwenda wapi?" Yesu akajibu, "Niendako huwezi kunifuata sasa, lakini utanifuata baadaye."
37 Petro akamwambia "Bwana, kwa nini siwezi kukufuata sasa? Niko tayari kufa kwa ajili yako!"
38 Yesu akajibu, "Je, uko tayari kweli kufa kwa ajili yangu? Kweli nakwambia, kabla jogoo hajawika utanikana mara tatu!"

 

John 14

 

 

1 Yesu aliwaambia, "Msifadhaike mioyoni mwenu. Mwaminini Mungu, niaminini na mimi pia.
2 Nyumbani mwa Baba yangu mna makao mengi; la sivyo ningalikwisha waambieni. Sasa nakwenda kuwatayarishieni nafasi.
3 Na nikienda na kuwatayarishieni nafasi, nitarudi na kuwachukueni kwangu, ili nanyi muwe pale nilipo mimi.
4 Mnajua njia ya kwenda huko ninakokwenda."
5 Thoma akamwuliza, "Bwana, hatujui unakokwenda, tutawezaje basi, kuijua hiyo njia?"
6 Yesu akamjibu, "Mimi ni njia, na ukweli na uzima. Hakuna awezaye kwenda kwa Baba ila kwa kupitia kwangu.
7 Ikiwa mnanijua mimi mnamjua na Baba yangu pia. Na tangu sasa, mnamjua, tena mmekwisha mwona."
8 Filipo akamwambia, "Bwana, tuonyeshe Baba, nasi tutatosheka."
9 Yesu akamwambia, "Filipo, nimekaa nanyi muda wote huu, nawe hujanijua? Aliyekwisha niona mimi amemwona Baba. Unawezaje basi, kusema: <Tuonyeshe Baba?>
10 Je, huamini kwamba mimi niko ndani ya Baba, naye Baba yuko ndani yangu? Maneno ninayowaambieni nyote siyasemi kwa mamlaka yangu; Baba aliye ndani yangu anafanya kazi yake.
11 Mnapaswa kuniamini ninaposema kwamba mimi niko ndani ya Baba naye Baba yuko ndani yangu. Ama sivyo, aminini kwa sababu ya mambo ninayofanya.
12 Kweli nawaambieni, anayeniamini atafanya mambo ninayofanya mimi; naam, atafanya hata makuu zaidi, maana nakwenda kwa Baba.
13 Na chochote mtakachoomba kwa jina langu nitafanya, ili Baba atukuzwe ndani ya Mwana.
14 Mkiniomba chochote kwa jina langu, nitawafanyieni.
15 "Mkinipenda mtazishika amri zangu.
16 Nami nitamwomba Baba naye atawapeni Msaidizi mwingine, atakayekaa nanyi milele.
17 Yeye ni Roho wa kweli. Ulimwengu hauwezi kumpokea kwa sababu hauwezi kumwona wala kumjua. Lakini ninyi mnamjua kwa sababu anabaki nanyi na yu ndani yenu.
18 "Sitawaacha ninyi yatima; nitakuja tena kwenu.
19 Bado kidogo nao ulimwengu hautaniona tena, lakini ninyi mtaniona; na kwa kuwa mimi ni hai, nanyi pia mtakuwa hai.
20 Siku ile itakapofika mtajua kwamba mimi niko ndani ya Baba, nanyi mko ndani yangu, nami ndani yenu.
21 Azipokeaye amri zangu na kuzishika, yeye ndiye anipendaye. Naye anipendaye mimi atapendwa na Baba yangu, nami nitampenda na kujidhihirisha kwake."
22 Yuda (si yule Iskarioti) akamwambia, "Bwana, itawezekanaje wewe kujidhihirisha kwetu na si kwa ulimwengu?"
23 Yesu akamjibu, "Mtu akinipenda atashika neno langu, na Baba yangu atampenda, nasi tutakuja kwake na kukaa naye.
24 Asiyenipenda hashiki maneno yangu. Na neno mlilosikia si langu, bali ni lake Baba aliyenituma.
25 "Nimewaambieni mambo haya nikiwa bado pamoja nanyi
26 lakini Msaidizi, Roho Mtakatifu, ambaye Baba atamtuma kwa jina langu, atawafundisheni kila kitu na kuwakumbusheni yote niliyowaambieni.
27 "Nawaachieni amani; nawapeni amani yangu. Siwapi ninyi kama vile ulimwengu ufanyavyo. Msiwe na wasiwasi, wala msifadhaike.
28 Mlikwisha sikia nikiwaambieni: <Ninakwenda zangu, kisha nitarudi tena kwenu.> Kama mngalinipenda mngalifurahi kwa sababu ninakwenda kwa Baba, maana yeye ni mkuu kuliko mimi.
29 Nimewaambieni haya sasa kabla hayajatokea, ili yatakapotokea mpate kuamini.
30 Sitasema nanyi tena mambo mengi, maana mtawala wa ulimwengu huu anakuja. Kwangu mimi hawezi kitu;
31 lakini ulimwengu unapaswa kujua kwamba nampenda Baba, na ndiyo maana nafanya kila kitu kama Baba alivyoniamuru. Simameni, tutoke hapa!"


go to chapters........1-7.......8-14.......15-18.......19-21

BOOK OF JOHN HOMEPAGE