John 15
1 "Mimi ni mzabibu wa kweli, na Baba yangu ndiye
mkulima.
2 Yeye huliondoa ndani yangu kila tawi lisilozaa matunda, na kila tawi
lizaalo hulisafisha lipate kuzaa zaidi.
3 Ninyi mmekwisha kuwa safi kwa sababu ya ule ujumbe niliowaambieni.
4 Kaeni ndani yangu, nami nikae ndani yenu. Tawi haliwezi peke yake kuzaa
matunda lisipokaa katika mzabibu hali kadhalika nanyi hamwezi kuzaa matunda
msipokaa ndani yangu.
5 "Mimi ni mzabibu, nanyi ni matawi yake. Akaaye ndani yangu, nami
ndani yake, huyo atazaa matunda mengi, maana bila mimi hamwezi kufanya
chochote.
6 Mtu yeyote asipokaa ndani yangu hutupwa nje kama tawi litupwalo nje hata
likakauka. Watu huliokota tawi la namna hiyo na kulitupa motoni liungue.
7 Mkikaa ndani yangu na maneno yangu yakikaa ndani yenu, basi, ombeni chochote
mtakacho nanyi mtapewa.
8 Baba yangu hutukuzwa kama mkizaa matunda mengi na kuwa wanafunzi wangu.
9 Mimi nimewapenda ninyi kama vile Baba alivyonipenda mimi. Kaeni katika
pendo langu.
10 Mkizishika amri zangu mtakaa katika pendo langu, kama vile nami nilivyozishika
amri za Baba yangu na kukaa katika pendo lake.
11 Nimewaambieni mambo haya ili furaha yangu ikae ndani yenu,
na furaha yenu ikamilike.
12 Hii ndiyo amri yangu: pendaneni; pendaneni kama nilivyowapenda ninyi.
13 Hakuna upendo mkuu zaidi kuliko upendo wa mtu atoaye uhai wake kwa ajili
ya rafiki zake.
14 Ninyi ni rafiki zangu mkifanya ninayowaamuru.
15 Ninyi siwaiti tena watumishi, maana mtumishi hajui anachofanya bwana
wake. Lakini mimi nimewaita ninyi rafiki, kwa sababu nimewajulisha yote
ambayo nimeyasikia kutoka kwa Baba yangu.
16 Ninyi hamkunichagua mimi; mimi niliwachagueni na kuwatuma mwende mkazae
matunda, matunda yadumuyo, naye Baba apate kuwapa ninyi chochote mumwombacho
kwa jina langu.
17 Basi, amri yangu kwenu ndiyo hii: pendaneni.
18 "Kama ulimwengu ukiwachukia ninyi, kumbukeni kwamba umenichukia
mimi kabla haujawachukia ninyi.
19 Kama mngalikuwa watu wa ulimwengu, ulimwengu ungaliwapenda ninyi kama
watu wake. Lakini kwa vile ninyi si wa ulimwengu, ila mimi nimewachagueni
kutoka ulimwenguni, kwa sababu hiyo ulimwengu unawachukieni.
20 Kumbukeni niliyowaambieni: mtumishi si mkuu zaidi kuliko bwana wake.
Ikiwa wamenitesa mimi, watawatesa na ninyi pia; kama wameshika neno langu,
watalishika na lenu pia.
21 Lakini hayo yote watawatendeeni ninyi kwa sababu ya jina langu, kwani
hawamjui yeye aliyenituma.
22 Kama nisingalikuja na kusema nao wasingalikuwa na hatia; lakini sasa
hawawezi kujitetea kwamba hawana dhambi.
23 Anayenichukia mimi, anamchukia na Baba yangu pia.
24 Kama nisingalifanya kwao mambo ambayo hakuna mtu mwingine amekwisha
yafanya wasingalikuwa na hatia; lakini sasa wameona niliyoyafanya wakinichukia
mimi, wakamchukia na Baba yangu pia.
25 Na hivi ni lazima yatimie yale yaliyoandikwa katika Sheria yao: <Wamenichukia
bure!>
26 "Atakapokuja huyo Msaidizi nitakayemtuma kwenu kutoka kwa Baba,
huyo Roho wa kweli atokaye kwa Baba, yeye atanishuhudia mimi.
27 Nanyi pia mtanishuhudia kwa kuwa mmekuwa nami tangu mwanzo.
John 16
1 "Nimewaambieni hayo kusudi msiiache imani yenu.
2 Watu watawatenga ninyi na masunagogi yao. Tena, wakati unakuja ambapo
kila atakayewaua ninyi atadhani anamhudumia Mungu.
3 Watawatendeeni mambo hayo kwa sababu hawamjui Baba, wala hawanijui mimi.
4 Basi, nimewaambieni mambo haya ili saa yake itakapofika mkumbuke kwamba
niliwaambieni. "Sikuwaambieni mambo haya tangu mwanzo kwa sababu nilikuwa
pamoja nanyi.
5 Lakini sasa namwendea yule aliyenituma; na hakuna hata mmoja wenu anayeniuliza:
<Unakwenda wapi?>
6 Kwa kuwa nimewaambieni mambo hayo mmejaa huzuni mioyoni mwenu.
7 Lakini, nawaambieni ukweli: afadhali kwenu mimi niende zangu, maana nisipokwenda
Msaidizi hatakuja kwenu. Lakini nikienda, basi, nitamtuma kwenu.
8 Naye atakapokuja atawathibitishia walimwengu kwamba wamekosea kuhusu
dhambi, uadilifu na hukumu ya Mungu.
9 Wamekosea kuhusu dhambi kwa sababu hawaniamini;
10 kuhusu uadilifu, kwa sababu naenda zangu kwa Baba, nanyi hamtaniona
tena;
11 kuhusu hukumu kwa sababu mkuu wa ulimwengu huu amekwisha hukumiwa.
12 "Ninayo bado mengi ya kuwaambieni, ila kwa sasa hamwezi kuyastahimili.
13 Lakini atakapokuja huyo Roho wa kweli atawaongoza kwenye ukweli wote;
maana hatasema kwa mamlaka yake mwenyewe, bali atawaambieni yote atakayosikia,
na atasema mambo yatakayokuwa yanakuja.
14 Yeye atanitukuza mimi kwa kuwa atawaambieni yale atakayopata kutoka
kwangu.
15 Vyote alivyo navyo Baba ni vyangu; ndiyo maana nimesema kwamba huyo
Roho Mtakatifu atawaambieni yale atakayopata kutoka kwangu.
16 "Bado kitambo kidogo nanyi hamtaniona; na baada ya
kitambo kidogo tena mtaniona!"
17 Hapo baadhi ya wanafunzi wake wakaulizana, "Ana maana gani anapotwambia:
<Bado kitambo kidogo nanyi hamtaniona; na baada ya kitambo kidogo tena
mtaniona?> Tena anasema: <Kwa kuwa ninakwenda kwa Baba!">
18 Basi, wakawa wanaulizana, "Ana maana gani anaposema: <Bado kitambo
kidogo?> Hatuelewi anaongelea nini."
19 Yesu alijua kwamba walitaka kumwuliza, basi akawaambia, "Je, mnaulizana
juu ya yale niliyosema: <Bado kitambo kidogo nanyi hamtaniona; na baada
ya kitambo kidogo tena mtaniona?>
20 Nawaambieni kweli, ninyi mtalia na kuomboleza, lakini ulimwengu utafurahi:
mtaona huzuni lakini huzuni yenu itageuka kuwa furaha.
21 Wakati mama anapojifungua huona huzuni kwa sababu saa ya maumivu imefika;
lakini akisha jifungua hayakumbuki tena maumivu hayo kwa sababu ya furaha
kwamba mtu amezaliwa duniani.
22 Ninyi pia mna huzuni sasa; lakini nitawajieni tena,
nanyi mtajaa furaha mioyoni mwenu, na furaha hiyo hakuna mtu atakayeiondoa
kwenu.
23 Siku hiyo hamtaniomba chochote. Kweli nawaambieni, chochote mtakachomwomba
Baba kwa jina langu, atawapeni.
24 Mpaka sasa hamjaomba chochote kwa jina langu. Ombeni nanyi mtapata ili
furaha yenu ikamilike.
25 "Nimewaambieni mambo hayo kwa mafumbo. Lakini wakati utakuja ambapo
sitasema tena nanyi kwa mafumbo, bali nitawaambieni waziwazi juu ya Baba.
26 Siku hiyo mtaomba kwa jina langu, na siwaambii kwamba nitamwomba Baba
kwa niaba yenu;
27 maana yeye mwenyewe anawapenda ninyi, kwa sababu ninyi mmenipenda mimi
na mmeamini kwamba nimetoka kwa Mungu.
28 Mimi nilitoka kwa Baba, nikaja ulimwenguni; na sasa nauacha ulimwengu
na kurudi kwa Baba."
29 Basi, wanafunzi wake wakamwambia, "Ahaa! Sasa unasema waziwazi
kabisa bila kutumia mafumbo.
30 Sasa tunajua kwamba wewe unajua kila kitu, na huna haja ya kuulizwa
maswali na mtu yeyote; kwa hiyo tunaamini kwamba umetoka kwa Mungu."
31 Yesu akawajibu, "Je, mnaamini sasa?
32 Wakati unakuja, tena umekwisha fika, ambapo ninyi nyote mtatawanyika
kila mtu kwake, nami nitaachwa peke yangu. Kumbe, lakini mimi siko peke
yangu, maana Baba yu pamoja nami.
33 Nimewaambieni mambo haya ili mpate kuwa na amani katika kuungana nami.
Ulimwenguni mtapata masumbuko; lakini jipeni moyo! Mimi nimeushinda ulimwengu!"
John 17
1 Yesu alipokwisha sema hayo, alitazama juu mbinguni,
akasema, "Baba, saa imefika! Mtukuze Mwanao ili naye Mwana apate kukutukuza.
2 Maana ulimpa Mwanao mamlaka juu ya watu wote ili awape uzima wa milele
wote hao uliompa.
3 Na uzima wa milele ndio huu: kukujua wewe uliye peke yako Mungu wa kweli,
na kumjua Yesu Kristo uliyemtuma.
4 Mimi nimekutukuza hapa duniani; nimeikamilisha ile kazi
uliyonipa nifanye.
5 Sasa, Baba, nitukuze mbele yako kwa ule utukufu niliokuwa nao kabla ya
kuumbwa ulimwengu.
6 "Nimekufanya ujulikane kwa watu wale ulionipa kutoka duniani. Walikuwa
watu wako, nawe ukanipa wawe wangu; nao wamelishika neno lako.
7 Sasa wanajua kwamba kila ulichonipa kimetoka kwako.
8 Mimi nimewapa ule ujumbe ulionipa nao wameupokea; wanajua kwamba kweli
nimetoka kwako, na wanaamini kwamba wewe ulinituma.
9 "Nawaombea hao; siuombei ulimwengu, ila nawaombea hao ulionipa,
maana ni wako.
10 Yote niliyo nayo ni yako, na yako ni yangu; na utukufu wangu umeonekana
ndani yao.
11 Na sasa naja kwako; simo tena ulimwenguni, lakini wao wamo ulimwenguni.
Baba Mtakatifu! Kwa nguvu ya jina lako ulilonipa, tafadhali uwaweke salama
ili wawe kitu kimoja kama sisi tulivyo mmoja.
12 Nilipokuwa nao, mimi niliwaweka salama kwa nguvu ya jina lako ulilonipa.
Mimi nimewalinda, wala hakuna hata mmoja wao aliyepotea, isipokuwa yule
aliyelazimika kupotea ili Maandiko Matakatifu yapate kutimia.
13 Basi, sasa naja kwako, na nimesema mambo haya ulimwenguni, ili waweze
kushiriki kikamilifu furaha yangu.
14 Mimi nimewapa neno lako, nao ulimwengu ukawachukia, kwa sababu wao si
wa ulimwengu kama vile nami nisivyo wa ulimwengu.
15 Siombi uwatoe ulimwenguni, bali naomba uwakinge na yule Mwovu.
16 Wao si wa ulimwengu, kama vile nami nisivyo wa ulimwengu.
17 Waweke wakfu kwa ukweli; neno lako ni ukweli.
18 Kama vile ulivyonituma ulimwenguni, nami pia nimewatuma wao ulimwenguni;
19 na kwa ajili yao mimi mwenyewe najiweka wakfu ili nao pia wafanywe wakfu
katika ukweli.
20 "Siwaombei hao tu, bali nawaombea pia wote watakaoamini kutokana
na ujumbe wao.
21 Naomba ili wote wawe kitu kimoja. Baba! Naomba wawe ndani
yetu kama vile wewe ulivyo ndani yangu nami ndani yako. Naomba wawe kitu
kimoja kusudi ulimwengu upate kuamini kwamba wewe ulinituma.
22 Mimi nimewapa utukufu uleule ulionipa mimi, ili wawe kitu kimoja kama
nasi tulivyo mmoja;
23 mimi niwe ndani yao, nawe uwe ndani yangu; naomba wakamilishwe na kuwa
kitu kimoja, ili ulimwengu upate kujua kwamba wewe ulinituma, na kwamba
unawapenda wao kama unavyonipenda mimi.
24 "Baba! Nataka wao ulionipa wawe pamoja nami pale nilipo, ili wauone
utukufu wangu ulionipa; kwa kuwa ulinipenda kabla ya kuumbwa ulimwengu.
25 Baba Mwema! Ulimwengu haukujui, lakini mimi nakujua. Hawa nao wanajua
kwamba wewe ulinituma.
26 Nimekufanya ujulikane kwao na nitaendelea kufanya hivyo, ili upendo
ulio nao kwangu uwe ndani yao, nami niwe ndani yao."
John 18
1 Yesu alipokwisha sema hayo, alikwenda ng'ambo ya kijito
Kedroni, pamoja na wanafunzi wake. Mahali hapo palikuwa na bustani, naye
Yesu akaingia humo pamoja na wanafunzi wake.
2 Yuda, aliyemsaliti Yesu, alipajua mahali hapo kwani mara nyingi Yesu
alikutana na wanafunzi wake huko.
3 Basi, Yuda alichukua kikosi cha askari na walinzi kutoka kwa makuhani
wakuu na Mafarisayo, akaja nao bustanini wakiwa na taa, mienge na silaha.
4 Yesu, hali akijua yote yatakayompata, akatokea, akawauliza, "Mnamtafuta
nani?"
5 Nao wakamjibu, "Yesu wa Nazareti!" Yesu akawaambia,
"Mimi ndiye." Msaliti Yuda alikuwa amesimama hapo pamoja nao.
6 Basi, Yesu alipowaambia: "Mimi ndiye", wakarudi nyuma, wakaanguka
chini.
7 Yesu akawauliza tena, "Mnamtafuta nani?" Wakamjibu, "Yesu
wa Nazareti!"
8 Yesu akawaambia, "Nimekwisha waambieni kwamba mimi ndiye. Basi,
kama mnanitafuta mimi, waacheni hawa waende zao."
9 (Alisema hayo ili yapate kutimia yale aliyosema: "Wale ulionipa
sikumpoteza hata mmoja.")
10 Simoni Petro alikuwa na upanga; basi, akauchomoa, akamkata sikio la
kulia mtumishi wa Kuhani Mkuu. Mtumishi huyo aliitwa Malko.
11 Basi, Yesu akamwambia Petro, "Rudisha upanga wako alani. Je, nisinywe
kikombe alichonipa Baba?"
12 Kile kikosi cha askari, mkuu wake na walinzi wa Wayahudi walimkamata
Yesu, wakamfunga
13 na kumpeleka kwanza kwa Anasi; Anasi alikuwa baba mkwe
wa Kayafa ambaye alikuwa Kuhani Mkuu mwaka huo.
14 Huyo Kayafa ndiye aliyekuwa amewashauri Wayahudi kwamba ni afadhali
mtu mmoja afe kwa ajili ya taifa.
15 Simoni Petro pamoja na mwanafunzi mwingine walimfuata Yesu. Huyo mwanafunzi
mwingine alikuwa anajulikana kwa Kuhani Mkuu, hivyo aliingia pamoja na
Yesu ndani ya ukumbi wa Kuhani Mkuu.
16 Lakini Petro alikuwa amesimama nje, karibu na mlango. Basi, huyo mwanafunzi
mwingine aliyekuwa anajulikana kwa Kuhani Mkuu alitoka nje akasema na mjakazi,
mngoja mlango, akamwingiza Petro ndani.
17 Huyo msichana mngoja mlango akamwuliza Petro, "Je, nawe pia ni
mmoja wa wanafunzi wa mtu huyu?" Petro akamwambia, "Si mimi!"
18 Watumishi na walinzi walikuwa wamewasha moto kwa sababu kulikuwa na
baridi, wakawa wanaota moto. Naye Petro alikuwa amesimama pamoja nao akiota
moto.
19 Basi, Kuhani akamwuliza Yesu juu ya wanafunzi wake na mafundisho yake.
20 Yesu akamjibu, "Nimesema na kila mtu daima hadharani. Kila mara
nimefundisha katika masunagogi na Hekaluni, mahali wakutanikiapo Wayahudi
wote; na wala sijasema chochote kwa siri.
21 Kwa nini waniuliza mimi? Waulize wale waliosikia nini niliwaambia. Wao
wanajua nilivyosema."
22 Alipokwisha sema hayo mlinzi mmoja aliyekuwa amesimama hapo akampiga
kofi akisema, "Je, ndivyo unavyomjibu Kuhani Mkuu?"
23 Yesu akamjibu, "Kama nimesema vibaya, onyesha huo ubaya; lakini
ikiwa nimesema vema, mbona wanipiga?"
24 Basi, Anasi akampeleka Yesu akiwa amefungwa, kwa Kuhani Mkuu Kayafa.
25 Petro alikuwa hapo akiota moto. Basi, wakamwuliza, "Je,
nawe pia si mmoja wa wanafunzi wake?" Yeye akakana na kusema, "Si
mimi!"
26 Mmoja wa watumishi wa Kuhani Mkuu, jamaa wa yule aliyekatwa sikio na
Petro, akamwuliza, "Je, mimi sikukuona wewe bustanini pamoja naye?"
27 Petro akakana tena; mara jogoo akawika.
28 Basi, walimchukua Yesu kutoka kwa Kayafa, wakampeleka ikulu. Ilikuwa
alfajiri, nao ili waweze kula Pasaka, hawakuingia ndani ya ikulu wasije
wakatiwa najisi.
29 Kwa hiyo, Pilato aliwaendea nje, akasema, "Mna mashtaka gani juu
ya mtu huyu?"
30 Wakamjibu, "Kama huyu hangalikuwa mwovu hatungalimleta
kwako."
31 Pilato akawaambia, "Haya, mchukueni ninyi wenyewe, mkamhukumu kufuatana
na Sheria yenu." Wayahudi wakamjibu, "Sisi hatuna mamlaka ya
kumwua mtu yeyote."
32 (Ilifanyika hivyo yapate kutimia maneno aliyosema Yesu kuonyesha atakufa
kifo gani.)
33 Pilato akaingia tena ndani ya ikulu, akamwita Yesu na kumwuliza: "Ati
wewe ndiye Mfalme wa Wayahudi?"
34 Yesu akamjibu, "Je, hayo ni maneno yako au wengine wamekwambia
habari zangu?"
35 Pilato akamjibu, "Je, ni Myahudi mimi? Taifa lako
na makuhani wamekuleta kwangu. Umefanya nini?"
36 Yesu akamjibu, "Ufalme wangu si wa ulimwengu huu. Kama ufalme wangu
ungekuwa wa ulimwengu huu watumishi wangu wangenipigania nisitiwe mikononi
mwa Wayahudi. Lakini sasa ufalme wangu si wa hapa."
37 Hapo Pilato akamwambia, "Basi, wewe ni Mfalme?" Yesu akajibu,
"Wewe umesema kwamba mimi ni Mfalme. Mimi nimezaliwa kwa ajili hiyo;
na kwa ajili hiyo nimekuja ulimwenguni kuwaambia watu juu ya ukweli. Kila
mtu wa ukweli hunisikiliza."
38 Pilato akamwambia, "Ukweli ni kitu gani?" Pilato alipokwisha
sema hayo, aliwaendea tena Wayahudi nje, akawaambia, "Mimi sioni hatia
yoyote kwake.
39 Lakini, mnayo desturi kwamba mimi niwafungulie mfungwa mmoja wakati
wa Pasaka. Basi, mwataka niwafungulieni Mfalme wa Wayahudi?"
40 Hapo wakapiga kelele: "La! Si huyu ila Baraba!" Naye Baraba
alikuwa mnyang'anyi.
go to chapters........1-7.......8-14.......15-18.......19-21