John 19

 

 

 

 

1 Basi, Pilato akaamuru Yesu achukuliwe, apigwe viboko.
2 Nao askari wakasokota taji ya miiba, wakamtia kichwani, wakamvika na joho la rangi ya zambarau.
3 Wakawa wanakuja mbele yake na kusema: "Shikamoo, Mfalme wa Wayahudi!" Wakampiga makofi.
4 Pilato akatoka tena nje, akawaambia, "Tazameni, namleta nje kwenu, mpate kujua kwamba mimi sikuona hatia yoyote kwake."
5 Basi, Yesu akatoka nje amevaa taji ya miiba na joho la rangi ya zambarau. Pilato akawaambia, "Tazameni! Mtu mwenyewe ni huyo."
6 Makuhani wakuu na walinzi walipomwona wakapaaza sauti: "Msulubishe! Msulubishe!" Pilato akawaambia, "Mchukueni basi, ninyi wenyewe mkamsulubishe, kwa maana mimi sikuona hatia yoyote kwake."
7 Wayahudi wakamjibu, "Sisi tunayo Sheria, na kufuatana na Sheria hiyo, ni lazima afe, kwa sababu alijifanya kuwa Mwana wa Mungu."
8 Pilato aliposikia maneno hayo akazidi kuogopa.


9 Basi, akaingia tena ndani ya ikulu, akamwuliza Yesu, "Umetoka wapi wewe?" Lakini Yesu hakumjibu neno.
10 Hivyo Pilato akamwambia, "Husemi nami? Je, hujui kwamba ninayo mamlaka ya kukufungua na mamlaka ya kukusulubisha?"

11 Yesu akamjibu, "Hungekuwa na mamlaka yoyote juu yangu kama hungepewa na Mungu. Kwa sababu hiyo, yule aliyenikabidhi kwako ana dhambi kubwa zaidi."
12 Tangu hapo, Pilato akawa anatafuta njia ya kumwachilia, lakini Wayahudi wakapiga kelele: "Ukimwachilia huyu mtu, wewe si rafiki yake Kaisari; kila mtu anayejifanya kuwa Mfalme humpinga Kaisari!"
13 Basi, Pilato aliposikia maneno hayo akamleta Yesu nje, akaketi juu ya kiti cha hukumu, mahali paitwapo: "Sakafu ya Mawe" (kwa Kiebrania, Gabatha).
14 Ilikuwa yapata saa sita mchana, siku ya maandalio ya Pasaka. Pilato akawaambia Wayahudi, "Tazameni, Mfalme wenu!"
15 Wao wakapaaza sauti: "Mwondoe! Mwondoe! Msulubishe!" Makuhani wakuu wakajibu, "Sisi hatuna Mfalme isipokuwa Kaisari!"
16 Basi, hapo Pilato akamtia Yesu mikononi mwao ili asulubiwe. Basi, wakamchukua Yesu.

17 Naye akatoka akiwa amejichukulia msalaba wake kwenda mahali paitwapo "Fuvu la Kichwa", (kwa Kiebrania Golgotha).

18 Hapo ndipo walipomsulubisha, na pamoja naye waliwasulubisha watu wengine wawili; mmoja upande wake wa kulia na mwingine upande wake wa kushoto, naye Yesu katikati.

19 Pilato aliandika ilani akaiweka juu ya msalaba. Nayo ilikuwa imeandikwa hivi: "Yesu wa Nazareti, Mfalme wa Wayahudi."
20 Wayahudi wengi waliisoma ilani hiyo, maana mahali hapo aliposulubiwa Yesu palikuwa karibu na mji. Tena ilani hiyo ilikuwa imeandikwa kwa Kiebrania, Kilatini, na Kigiriki.
21 Basi, makuhani wakuu wakamwambia Pilato, "Usiandike: <Mfalme wa Wayahudi>, ila <Yeye alisema, Mimi ni Mfalme wa Wayahudi.">
22 Pilato akajibu, "Niliyoandika, nimeandika!"
23 Askari walipokwisha msulubisha Yesu, walizichukua nguo zake, wakazigawa mafungu manne, fungu moja kwa kila askari. Walichukua pia na kanzu yake; kanzu hiyo ilikuwa imefumwa kwa kipande kimoja tu, bila mshono.
24 Basi, hao askari wakashauriana: "Tusiipasue, ila tuipigie kura itakuwa ya nani." Jambo hilo lilifanyika ili yatimie Maandiko Matakatifu yasemayo: "Waligawana mavazi yangu, na nguo yangu wakaipigia kura." Basi, ndivyo walivyofanya hao askari.


25 Karibu na msalaba wake Yesu walikuwa wamesimama mama yake, na dada ya mama yake, Maria mke wa Kleopa, na Maria Magdalene.
26 Yesu alipomwona mama yake, na karibu naye amesimama yule mwanafunzi aliyempenda, akamwambia mama yake: "Mama! Tazama, huyo ndiye mwanao."
27 Halafu akamwambia yule mwanafunzi: "Tazama, huyo ndiye mama yako." Na tangu saa ile huyo mwanafunzi alimchukua akae nyumbani kwake.

28 Yesu alijua kwamba yote yalikuwa yametimia; na, ili Maandiko Matakatifu yapate kutimia, akasema, "Naona kiu."
29 Hapo palikuwa na bakuli limejaa siki. Basi, wakachovya sifongo katika hiyo siki, wakaitia juu ya ufito wa husopo, wakamwekea mdomoni.
30 Yesu alipokwisha pokea hiyo siki, akasema, "Yametimia!" Kisha akainama kichwa, akatoa roho.

31 Ilikuwa Ijumaa, siku ya Maandalio. Kwa hiyo, kusudi miili isikae msalabani siku ya Sabato, maana siku hiyo ya Sabato ilikuwa siku kubwa, Wayahudi walimwomba Pilato miguu ya hao waliosulubiwa ivunjwe na miili yao iondolewe.


32 Basi, askari walikwenda, wakaivunja miguu ya yule mtu wa kwanza na yule wa pili ambao walikuwa wamesulubiwa pamoja na Yesu.
33 Lakini walipomfikia Yesu waliona kwamba alikwisha kufa, na hivyo hawakumvunja miguu.
34 Lakini askari mmoja alimtoboa ubavuni kwa mkuki, na mara ikatoka damu na maji.
35 (Naye aliyeona tukio hilo ametoa habari zake ili nanyi mpate kuamini. Na hayo aliyosema ni ukweli, tena yeye anajua kwamba anasema ukweli.)
36 Jambo hilo lilitendwa ili Maandiko Matakatifu yatimie: "Hapana hata mfupa wake mmoja utakaovunjwa."
37 Tena Maandiko mengine yanasema: "Watamtazama yule waliyemtoboa."
38 Baada ya hayo, Yosefu, mwenyeji wa Armathaya, alimwomba Pilato ruhusa ya kuuchukua mwili wa Yesu. (Yosefu alikuwa mfuasi wa Yesu, lakini kwa siri, maana aliwaogopa viongozi wa Wayahudi). Basi, Pilato akamruhusu. Hivyo Yosefu alikwenda, akauondoa mwili wa Yesu.
39 Naye Nikodemo ambaye hapo awali alikuwa amemwendea Yesu usiku, akaja akiwa amechukua mchanganyiko wa manemane na ubani kiasi cha kilo thelathini.
40 Basi, waliutwaa mwili wa Yesu, wakaufunga sanda pamoja na manukato kufuatana na desturi ya Wayahudi katika kuzika.
41 Mahali hapo aliposulubiwa Yesu palikuwa na bustani, na katika bustani hiyo kulikuwa na kaburi jipya ambalo hakutiwa bado mtu yeyote ndani yake.
42 Basi, kwa sababu ya shughuli za Wayahudi za maandalio ya Sabato, na kwa vile kaburi hilo lilikuwa karibu, wakamweka Yesu humo.


John 20

 

 

 

1 Alfajiri na mapema Jumapili, kukiwa bado na giza, Maria Magdalene alikwenda kaburini, akaliona lile jiwe limeondolewa mlangoni pa kaburi.
2 Basi, akaenda mbio hadi kwa Petro na yule mwanafunzi mwingine ambaye Yesu alimpenda, akawaambia, "Wamemwondoa Bwana kaburini, na wala hatujui walikomweka."
3 Petro pamoja na yule mwanafunzi mwingine wakaenda kaburini.
4 Wote wawili walikimbia lakini yule mwanafunzi mwingine alikimbia mbio zaidi kuliko Petro, akatangulia kufika kaburini.
5 Alipoinama na kuchungulia ndani, aliona sanda, lakini hakuingia ndani.
6 Simoni Petro naye akaja akimfuata, akaingia kaburini; humo akaona sanda,
7 na kile kitambaa alichofungwa Yesu kichwani. Hicho kitambaa hakikuwekwa pamoja na hiyo sanda, bali kilikuwa kimekunjwa na kuwekwa mahali peke yake.
8 Kisha yule mwanafunzi mwingine aliyemtangulia kufika kaburini, akaingia pia ndani, akaona, akaaamini.


9 (Walikuwa bado hawajaelewa Maandiko Matakatifu yaliyosema kwamba ilikuwa lazima afufuke kutoka wafu).


10 Basi, hao wanafunzi wakarudi nyumbani.
11 Maria alikuwa amesimama nje ya kaburi, akilia. Huku akiwa bado analia, aliinama na kuchungulia kaburini,
12 akawaona malaika wawili waliovaa mavazi meupe, wameketi pale mwili wa Yesu ulipokuwa umelazwa, mmoja kichwani na wa pili miguuni.


13 Hao malaika wakamwuliza, "Mama, kwa nini unalia?" Naye akawaambia, "Wamemwondoa Bwana wangu, na wala sijui walikomweka!"
14 Baada ya kusema hayo, aligeuka nyuma, akamwona Yesu amesimama hapo, lakini asitambue ya kuwa ni Yesu.
15 Yesu akamwuliza, "Mama, kwa nini unalia? Unamtafuta nani?" Maria, akidhani kwamba huyo ni mtunza bustani, akamwambia, "Mheshimiwa, kama ni wewe umemwondoa, niambie ulikomweka, nami nitamchukua."


16 Yesu akamwambia, "Maria!" Naye Maria akageuka, akamwambia kwa Kiebrania, "Raboni" (yaani "Mwalimu").
17 Yesu akamwambia, "Usinishike; sijakwenda bado juu kwa Baba. Lakini nenda kwa ndugu zangu uwaambie: nakwenda juu kwa Baba yangu na Baba yenu, Mungu wangu na Mungu wenu."
18 Hivyo Maria Magdalene akaenda akawapa habari wale wanafunzi kuwa amemwona Bwana, na kwamba alikuwa amemwambia hivyo.
19 Ilikuwa jioni ya siku hiyo ya Jumapili. Wanafunzi walikuwa wamekutana pamoja ndani ya nyumba, na milango ilikuwa imefungwa kwa sababu waliwaogopa viongozi wa Wayahudi. Basi, Yesu akaja, akasimama kati yao, akawaambia, "Amani kwenu!"
20 Alipokwisha sema hayo, akawaonyesha mikono yake na ubavu wake. Basi, hao wanafunzi wakafurahi mno kumwona Bwana.
21 Yesu akawaambia tena, "Amani kwenu! Kama vile Baba alivyonituma mimi, nami nawatuma ninyi."
22 Alipokwisha sema hayo, akawapulizia na kuwaambia, "Pokeeni Roho Mtakatifu.
23 Mkiwasamehe watu dhambi zao, wamesamehewa; msipowaondolea, hawasamehewi."
24 Thoma mmoja wa wale kumi na wawili (aitwaye Pacha), hakuwa pamoja nao wakati Yesu alipokuja.
25 Basi, wale wanafunzi wengine wakamwambia, "Tumemwona Bwana." Thoma akawaambia, "Nisipoona mikononi mwake alama za misumari, na kutia kidole changu katika kovu hizo, na kutia mkono wangu ubavuni mwake, sitasadiki."
26 Basi, baada ya siku nane hao wanafunzi walikuwa tena pamoja mle ndani, na Thoma alikuwa pamoja nao. Milango ilikuwa imefungwa, lakini Yesu akaja, akasimama kati yao, akasema, "Amani kwenu!"
27 Kisha akamwambia Thoma, "Lete kidole chako hapa uitazame mikono yangu; lete mkono wako ukautie ubavuni mwangu. Usiwe na mashaka, ila amini!"


28 Thoma akamjibu, "Bwana wangu na Mungu wangu!"
29 Yesu akamwambia, "Je, unaamini kwa kuwa umeniona? Heri yao wale ambao hawajaona, lakini wameamini."
30 Yesu alifanya mbele ya wanafunzi wake ishara nyingine nyingi ambazo hazikuandikwa katika kitabu hiki.
31 Lakini hizi zimeandikwa ili mpate kuamini kwamba Yesu ni Kristo, Mwana wa Mungu; na kwa kuamini mpate kuwa na uzima kwa nguvu ya jina lake.

 

John 21

 

 

1 Baada ya hayo Yesu aliwatokea tena wanafunzi wake kando ya ziwa Tiberia. Aliwatokea hivi:
2 Simoni Petro, Thoma (aitwaye Pacha), na Nathanieli mwenyeji wa Kana Galilaya, wana wawili wa Zebedayo na wanafunzi wake wengine wawili, walikuwa wote pamoja.
3 Simoni Petro aliwaambia, "Nakwenda kuvua samaki." Nao wakamwambia, "Nasi tutafuatana nawe." Basi, wakaenda, wakapanda mashua, lakini usiku huo hawakupata chochote.
4 Kulipoanza kupambazuka, Yesu alisimama kando ya ziwa, lakini wanafunzi hawakujua kwamba alikuwa yeye.
5 Basi, Yesu akawauliza, "Vijana, hamjapata samaki wowote sio?" Wao wakamjibu, "La! Hatujapata kitu."
6 Yesu akawaambia, "Tupeni wavu upande wa kulia wa mashua nanyi mtapata samaki." Basi, wakatupa wavu lakini sasa hawakuweza kuuvuta tena kwa wingi wa samaki.
7 Hapo yule mwanafunzi aliyependwa na Yesu akamwambia Petro, "Ni Bwana!" Simoni Petro aliposikia ya kuwa ni Bwana, akajifunga vazi lake (maana hakuwa amelivaa), akarukia majini.
8 Lakini wale wanafunzi wengine walikuja pwani kwa mashua huku wanauvuta wavu uliojaa samaki; hawakuwa mbali na nchi kavu, ila walikuwa yapata mita mia moja kutoka ukingoni.
9 Walipofika nchi kavu waliona moto wa makaa umewashwa na juu yake pamewekwa samaki na mkate.
10 Yesu akawaambia, "Leteni hapa baadhi ya samaki mliovua."
11 Basi, Simoni Petro akapanda mashuani, akavuta hadi nchi kavu ule wavu uliokuwa umejaa samaki wakubwa mia moja na hamsini na watatu. Na ingawa walikuwa wengi hivyo wavu haukukatika.
12 Yesu akawaambia, "Njoni mkafungue kinywa." Hakuna hata mmoja wao aliyethubutu kumwuliza: "Wewe ni nani?" Maana walijua alikuwa Bwana.
13 Yesu akaja, akatwaa mkate akawapa; akafanya vivyo hivyo na wale samaki.
14 Hii ilikuwa mara ya tatu Yesu kuwatokea wanafunzi wake baada ya kufufuka kutoka wafu.
15 Walipokwisha kula, Yesu alimwuliza Simoni Petro, "Simoni, mwana wa Yohane! Je, wanipenda mimi zaidi kuliko hawa?" Naye akajibu, "Naam, Bwana; wajua kwamba mimi nakupenda." Yesu akamwambia, "Tunza wana kondoo wangu."


16 Kisha akamwambia mara ya pili, "Simoni mwana wa Yohane! Je, wanipenda?" Petro akamjibu, "Naam, Bwana; wajua kwamba nakupenda." Yesu akamwambia, "Tunza kondoo wangu."
17 Akamwuliza mara ya tatu, "Simoni mwana wa Yohane! Je, wanipenda?" Hapo Petro akahuzunika kwa sababu alimwuliza mara ya tatu: "Wanipenda?" akamwambia, "Bwana, wewe wajua yote; wewe wajua kwamba mimi nakupenda." Yesu akamwambia, "Tunza kondoo wangu!
18 Kweli nakwambia, ulipokuwa kijana ulizoea kujifunga mshipi na kwenda kokote ulikotaka. Lakini utakapokuwa mzee utanyosha mikono yako, na mtu mwingine atakufunga na kukupeleka usikopenda kwenda."
19 (Kwa kusema hivyo, alionyesha jinsi Petro atakavyokufa na kumtukuza Mungu.) Kisha akamwambia, "Nifuate."
20 Hapo Petro akageuka, akamwona yule mwanafunzi ambaye Yesu alimpenda, anafuata (Huyu mwanafunzi ndiye yule ambaye wakati wa chakula cha jioni, alikaa karibu sana na Yesu na kumwuliza: "Bwana ni nani atakayekusaliti?")
21 Basi, Petro alipomwona huyo akamwuliza Yesu, "Bwana, na huyu je?"
22 Yesu akamjibu, "Kama nataka abaki mpaka nitakapokuja, yakuhusu nini? Wewe nifuate mimi."
23 Basi, habari hiyo ikaenea miongoni mwa wale ndugu kwamba mwanafunzi huyo hafi. Lakini Yesu hakumwambia kwamba mwanafunzi huyo hafi, ila, "Kama nataka abaki mpaka nitakapokuja, yakuhusu nini?"
24 Huyo ndiye yule aliyeshuhudia mambo haya na kuyaandika. Nasi twajua kwamba aliyoyasema ni kweli.
25 Kuna mambo mengine mengi aliyofanya Yesu, ambayo kama yangeandikwa yote, moja baada ya lingine, nadhani hata ulimwengu wenyewe usingetosha kuviweka vitabu ambavyo vingeandikwa.



 

go to chapters........1-7.......8-14.......15-18.......19-21

BOOK OF JOHN HOMEPAGE